Italia yapendezwa na sera za Tanzania yataka kuwekeza kwenye kaboni
Serikali ya Italia imeonesha nia ya kufanya uwekezaji katika biashara ya kaboni na hifadhi ya mazingira.
Hayo yamebainika kwenye mazungumzo kati ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa wa Nchi za Ulaya, Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ya Italia Bi. Ambra Migliorisi. Mkurugenzi huyo wa uhusiano aliambatana na Naibu Mtendaji Mkuu wa Shirika la kimataifa la Sustainable Energy for All (SEforALL) lenye makao makuu jijini Vienna, Austria Bw. Stefano Marguccio.
Maungumzo hayo yaliyofanyika Juni 14, 2026, jijini Bonn, Ujerumani wakati wa Mkutano wa 64 wa Kamati za Utekelezaji na Sayansi na Ushauri chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ukiendelea.
Mkurugenzi huyo alisema taifa lake linataka kukuza ushirikiano na Tanzania kwani wamevutiwa na mazingira yaliyopo ya uwekezaji nchini.
Bi. Ambra alisema Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ya nchini humo imeonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania kwenye biashara ya kaboni hasa katika utekelezaji wa Ibara ya 6.2 ya Mkataba wa Paris kuhusu kuhusu ushirikiano wa utekelezaji wa biashara ya kaboni.
''Kati ya nchi 14 zilizoainishwa barani Afrika, Tanzania imechaguliwa na kupewa kipaumbele katika uwekezaji huo kutokana na uwepo wa Sera, Kanuni, Miongozo na mifumo mizuri ya uendeshaji wa Biashara ya Kaboni pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo'' alisema Bi. Ambra.
Sanjari na hilo, Serikali ya Italia kupitia Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ambayo imedhamiria kuwekeza kwa kuanza na miradi ya majaribio kwa kushirikiana na Mtaalamu Elekezi kutoka Shirika la SEforALL aliyepewa kandarasi ya kufanya upembuzi yakinifu utakaowezesha kufanyika kwa uwekezaji huo.
Dkt. Muyungi, aliishukuru Serikali ya Italia kupitia wizara hiyo kwa kuendeleza na kukuza ushirikiano na uhusiano wa miaka mingi na kuikaribisha kuwekeza nchini kwakuwa masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira yamepewa kipaumbele katika nguzo ya tatu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema biashara ya kaboni ni mojawapo ya maeneo ya kipaumbele katika kuongeza mapato ya nchi kupitia shabaha iliyowekwa kwenye Dira 2050 ya ukusanyaji wa Dola za Kimarekani bilioni mbili katika eneo la biashara hiyo pamoja na Uchumi wa Buluu, hivyo ili kufikia lengo hilo ni muhimu kufanyika jitihada mahsusi katika kuongeza na kukuza ushirikiano na uhusiano na nchi mbalimbali ili kupata wawekezaji wengi.
Pia, Dkt. Muyungi alihimiza Serikali ya Italia kuanza mara moja mchakato na mawasiliano rasmi kupitia Wizara ya Mambo ya Njena Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuharakisha mchakato wa uwekezaji huo.
Mkutano huo unafanyika kuanzia Juni 8 hadi 18, 2026 ukiwakutanisha wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi kutoka katika nchi zote wanachama wa mkataba huo kujadili na kukubaliana misimamo ya nchi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali ya majadiliano kuendana na makundi ya Afrika na nchi zinazoendelea.

Post a Comment