RIO FERDINAND APOKEWA DAR KWA KISHINDO




Nahodha na mchezaji wa zamani wa klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya England, Rio Ferdinand, amelakiwa na umati mkubwa wa mashabiki wa soka waliofurika kwa wingi katika Uwanja wa Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam. 

Nguli huyo alilakiwa kwa shamrashamra za aina yake zilizosindikizwa na ngoma za kiasili, michezo ya sarakasi, pamoja na uwepo wa wachezaji chipukizi kutoka akademi mbalimbali za michezo hapa nchini, hatua iliyolenga kuonesha furaha na heshima kubwa ya watanzania kwa ujio wa mchezaji huyo mwenye jina kubwa duniani.

Rio Ferdinand, aliyewasili nchini Mei 19, 2026 kwa ziara maalum ya siku nne kufuatia mwaliko rasmi wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, alikiri kuwa hakutarajia mapokezi hayo makubwa wakati alipopata nafasi ya kuongea na watanzania waliofurika uwanja wa ndege kumpokea.

Rio Ferdinand alieleza kuguswa na mapokezi hayo ya kifalme na kuweka wazi kuwa ana hamu kubwa ya kujifunza zaidi kuhusu utamaduni wa Tanzania, kukutana na wananchi, na kuona namna ushirikiano wa kimichezo unavyoweza kufungua fursa mpya kwa vijana wenye shauku. 










Katika ziara yake inayotarajiwa kuhitimishwa Mei 22, nyota huyo atajumuika katika shughuli mbalimbali zikiwemo kutembelea akademi za vijana, kukutana na wadau wa michezo, na kutembelea vivutio vya utalii nchini, hatua inayotajwa na mashabiki wengi waliojitokeza uwanjani hapo kuwa itaongeza hamasa kubwa ya soka nchini kuelekea michuano ya AFCON.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi mkono wa heri kwa nyota huyo aliyepata mafanikio makubwa chini ya kocha Sir Alex Ferguson, Waziri Paul Makonda amesema kuwa mapokezi hayo makubwa na uwepo wa Ferdinand nchini ni ishara tosha ya kuonesha ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi huru, salama, na ipo tayari kwa asilimia mia moja kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika ya mwaka 2027 (AFCON 2027). 

Makonda alisisitiza kuwa mikakati hii yote inafanyika chini ya maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayepigania kwa dhati maendeleo ya vijana, akibainisha kuwa kupitia ujio wa mastaa kama Rio Ferdinand na Didier Drogba, dunia itazidi kuifahamu Tanzania na kutambua vipaji vikubwa vilivyopo nchini.

No comments