Kauli ya Dangote inakumbusha Watanzania kuiunga Mkono Serikali katika Kulinda Amani

 


Tahariri ya gazeti la HabariLeo inaitazama ziara ya hivi karibuni ya mfanyabiashara bilionea namba moja barani Afrika, Aliko Dangote, nchini Tanzania kama kielelezo kikubwa cha mafanikio ya diplomasia ya kiuchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Akiongoza ujumbe wake katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Dangote alitoa pongezi za dhati kwa serikali kwa namna ilivyoboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akimshukuru Rais Samia kwa kutatua changamoto nyingi zilizokuwa zikikabili Kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara. 

Hatua hiyo imethibitisha ahadi ya Rais Samia ya kulinda uwekezaji, jambo ambalo limeongeza tija na ufanisi wa uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa moja ya maeneo makuu na ya kimkakati kwa uwekezaji wa kampuni ya Dangote Group barani Afrika.

Habari njema zaidi iliyotokana na mazungumzo hayo ni nia ya Dangote kuingia ubia na Serikali ya Tanzania katika mradi mkubwa wa kusafisha mafuta ghafi unaokadiriwa kugharimu dola bilioni 17, sawa na takriban shilingi trilioni 44.2 za Kitanzania. 

Mradi huu mkubwa unatajwa kuwa na manufaa makubwa si tu kwa Tanzania bali kwa nchi zote za Afrika Mashariki na Ethiopia, kwani utasaidia kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje ya bara la Afrika, kupunguza athari za misukosuko ya bei katika soko la dunia, na kufungua milango ya umiliki wa hisa kwa nchi za ukanda huu.

Mhariri anabainisha kuwa fursa hii kubwa inakuja hapa nchini kutokana na uaminifu mkubwa wa taifa la Tanzania, na inazima kabisa upotoshaji uliokuwa ukifanywa na baadhi ya nchi jirani zilizokuwa zikitafuta mradi huo kwa maslahi yao wenyewe.

Kutokana na ukweli huo, ni thibitisho tosha kuwa Rais Samia anafanya kazi kubwa inayotambulika kimataifa katika kuvutia mitaji. 

Sifa hii kubwa ya kuwa eneo salama na mahali sahihi pa uwekezaji ni tunu ambayo kila Mtanzania anapaswa kuilinda kwa wivu mkubwa kwa kudumisha amani, utulivu, usalama na ukarimu ambao ndio nguzo kuu zinazovutia wawekezaji hawa.

Mhariri anatoa mwito kwa jamii kumuunga mkono kwa dhati Rais Samia na serikali yake, kwa kudumisha amani huku akihimiza mamlaka husika kuendelea kuondoa vikwazo vya kiutawala vinavyorudisha nyuma uwekezaji, ili kuweka mazingira bora zaidi yatakayofanya Watanzania waendelee kuona ufahari wa nchi yao na kuwa walinzi wakuu wa amani na maendeleo.

No comments