KAMATI YA BUNGE YAITAKA SERIKALI KUIPATIA BOHARI YA DAWA (MSD) MTAJI WA SHILINGI BILIONI 300




Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeitaka Serikali kuipatia Bohari ya Dawa (MSD) mtaji wa kiasi cha shilingi bilioni 300 ili kuinusuru na changamoto ya ukosefu wa mtaji na madeni inayoidai serikali. 

Katika taarifa iliyowasilishwa bungeni Mei 11, 2026 na kutiwa saini na mwenyekiti wa Kamati  Johannes Lukumay imebainisha kuwa pamoja na juhudi za serikali kujenga maghala makubwa ya kisasa mkoani Dodoma na Mtwara kwa gharama ya shilingi bilioni 42.3, bado MSD inahitaji msukumo mkubwa wa kifedha ili iweze kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa huduma za dawa na vifaa tiba nchini. 

Kamati imesisitiza kuwa kiasi hicho cha fedha kitasaidia kuimarisha uwezo wa bohari hiyo katika ununuzi wa bidhaa za afya kwa wingi na kwa gharama nafuu, jambo ambalo ni mhimili wa ustawi wa sekta ya afya kwa wananchi wote.

Uchambuzi wa Kamati kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/2026 umebaini kuwa upatikanaji wa fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo bado ni wa kusuasua, hali inayochelewesha ukamilishaji wa miundombinu muhimu ya afya. 

Hadi kufikia mwezi Februari 2026, ni asilimia 46 tu ya fedha za ndani za maendeleo zilizokuwa zimetolewa, huku miradi 41 kati ya 58 ikiwa haijapokea kiasi chochote cha fedha. Hali hii imeathiri miradi ya kimkakati kama ujenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (New Muhimbili) na ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali mbalimbali za rufaa za mikoa, jambo ambalo Kamati imeshauri serikali kulishughulikia kwa uharaka kabla ya mwaka wa fedha haujaisha.

Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Afya imetengewa jumla ya shilingi trilioni 1.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia mbili ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita. 

Kamati imepongeza ongezeko hilo lakini imeelezea wasiwasi wake juu ya kupungua kwa makadirio ya makusanyo ya maduhuli kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya wizara kwa asilimia tisa. 

Ili kuhakikisha huduma za afya zinaimarika, Kamati imetoa rai kwa serikali kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato ili kuzuia uvujaji na kuhakikisha kuwa kila shilingi inayokusanywa inatumika kuboresha huduma za ubingwa bobezi na kupunguza uhaba wa wataalamu wa tiba mionzi na madaktari bingwa.

Kamati katika taarifav yake imesisitiza kuwa uimarishaji wa MSD na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ni kielelezo cha uwajibikaji wa haki unaolenga kulinda afya za Watanzania. Kupitia usimamizi madhubuti na utoaji wa fedha za miradi kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa, taifa litaweza kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora za afya na kuimarisha tiba utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


No comments