JAJI CHANDE NA KATAZO LA KAFARA
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani Oktoba 29 , Jaji Othman Chande, amebainisha kuwa katika mchakato wa kukusanya maoni, wananchi wengi wamewasilisha hitaji la kuwepo kwa uwajibikaji kwa wale wote waliohusika na uvunjifu wa amani, huku wakisisitiza kuwa hatua hizo lazima zizingatie misingi ya kisheria.
Aidha Jaji Chande amefafanua kuwa maoni hayo yameelekeza kuwa yeyote anayestahili kuwajibishwa afanyiwe hivyo kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini kukiwa na tahadhari kubwa kuwa asitolewe mtu kafara ili tu kuridhisha matakwa ya watu fulani au kutuliza shinikizo.
Msisitizo huo wa tume unalenga kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila upendeleo wala kulazimisha lawama kwa watu wasiohusika, jambo ambalo limepokelewa na wadau kama msingi imara wa kuelekea kwenye maridhiano ya kweli na ya kudumu.
Wakati huohuo, kufuatia ripoti hiyo, kumeibuka mjadala mpana unaoashiria kuwa Watanzania wengi wanaamini kuwa amani ndiyo dira na msingi wa maendeleo, hivyo wananchi wanashauriwa kuwa wavumilivu wakati wakisubiri hatua zinazofuata, ikiwemo kuwapo kwa Tume ya Uchunguzi wa Jinai.
Waumini wa demokrasia na haki za binadamu wamekumbushwa kuwa tayari kusikiliza maoni ya wengine na kutambua kuwa kupata haki hakupaswi kuingilia au kupora haki za watu wengine.
Kwa ujumla, sauti za umoja zimeendelea kupazwa zikihimiza kuwa amani inapotoweka hata hiyo haki inayotafutwa haiwezi kupatikana, hivyo kila mmoja anapaswa kusimama kwa pamoja kuilinda amani kama desturi ya taifa huku mchakato wa kuwajibishana kwa haki ukiendelea.

Post a Comment