MAFUNZO YA UANAGENZI NA MKAKATI WA UZALISHAJI AJIRA NCHINI
Ujenzi wa miundombinu ya maji, upatikanaji wa bima za afya, na upatikanaji wa ujuzi wa vitendo na nadharia ni miongoni mwa manufaa makubwa ambayo wanafunzi wamepata kutokana na mafunzo ya Uanagenzi yanayodhaminiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano kwa mwaka 2025/26, katika Chuo cha Ufundi Mtawanya kilichopo Manispaa ya Mtwara.
Aidha, kutokana na mafunzo hayo wanafunzi wa fani ya ufundi bomba wameweza kusambaza mabomba ya maji kwenye majengo ya chuo hicho ikiwemo vyoo na hosteli, huku utaratibu wa bima ya afya uliofanywa na Serikali kupitia fedha wanazolipa chuoni ukiwa umesaidia kuongeza morali ya masomo na kupunguza gharama kwa wazazi.
Aidha, Serikali inatoa fedha za ununuzi wa vifaa vya mafunzo, hatua inayowafanya wanagenzi hao kupata ujuzi thabiti chini ya usimamizi wa wakufunzi wao.
Mkuu wa Chuo hicho, Mwalimu Sophia Mkopi, amebainisha kuwa kumekuwa na mahitaji makubwa sana ya vijana katika programu hii ya nane ya mafunzo ambapo walipokea maombi zaidi ya 500, lakini kutokana na mgao wa Wizara walipatiwa vijana 100 pekee waliosambazwa kwenye fani tano za ufundi.
Chuo hiki ambacho kilianzishwa mwaka 1975 chini ya Wizara ya Elimu kwa lengo la kutoa mafunzo ya ufundi stadi na malezi ya kuongeza ujuzi, kwa sasa kimekuwa chachu ya mabadiliko kupitia mfumo huu wa uanagenzi ambao unalenga kuwajengea uwezo wananchi, hususan vijana.
Baadhi ya wanafunzi wa uanagenzi chuoni hapo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kujenga ujuzi na kujiamini, ambapo mwanagenzi wa ufundi bomba mwenye umri wa miaka 21, Jesca Albeto Mtonya, alisimulia namna anavyomudu mifumo ya umwagiliaji maji mashambani kwa njia ya mabomba na jinsi ujuzi huo unavyomsaidia kufanya kazi ndogondogo kwa sasa.
Wakufunzi chuoni hapo, akiwemo Sofia Hamis Lingondo wa ufundi wa magari, walithibitisha kuwa programu hii inawaandaa vyema vijana, akitolea mfano maisha yake mwenyewe ambapo alisoma uanagenzi hapo chuoni, akaenda kujiendeleza juu na kisha kurejea Mtawanya kama mkufunzi kamili.
Mratibu wa Mafunzo ya Uanagenzi, Kelvin Ndunguru, aliongeza kuwa uwepo wa vijana hao 100 wa kozi ya muda mfupi umetoa mchango mkubwa katika kuboresha chuo kwani kupitia miradi ya vitendo wameweza kutekeleza majukumu ya ufundi bomba, uchomeleaji, na ufundi magari.
Jitihada hizi zote ni sehemu ya Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano yenye lengo la kuhakikisha nguvukazi ya nchi inapata ujuzi stahiki wa kujiajiri na kuajiriwa ndani na nje ya nchi, ambapo kwa sasa jumla ya vijana 5,746 wanapatiwa mafunzo haya ya uanagenzi katika vyuo 46 nchini kote.




Post a Comment