BBT-UVUVI: MAPINDUZI YA AJIRA NA FAHARI YA UCHUMI WA BLUU KWA VIJANA
Manung’uniko ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana sasa yanapata jibu madhubuti kupitia uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta ya uvuvi, hatua inayothibitisha kuwa fursa za kujiajiri ni nyingi pale nyenzo na maarifa vinapokutana.
Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) imekuwa mhimili wa mabadiliko haya, ikionyesha kuwa suluhu ya ajira haiko kwenye makaratasi pekee bali kwenye utajiri wa rasilimali za maji nchini.
Katika kufaniklisha hilo serikali imetoa mkopo wa Sh bilioni saba kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya vijana 308 waliohitimu mafunzo ya vitendo, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kulitegemeza taifa badala ya kubaki kuwa watazamaji katika ukuaji wa uchumi.
Katika Kanda ya Ziwa, mikoa ya Mwanza, Mara, na Kagera imekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa na wanufaika zaidi ya 100 wanaopatiwa vitendea kazi vya kisasa ikiwemo vizimba na vifaranga vya samaki.
Mpango huu haujaishia kwenye samaki pekee, bali umepanua mnyororo wa thamani hadi kwenye kilimo cha mwani, ufugaji wa majongoo bahari, na kunenepesha kaa katika maeneo ya maji chumvi, hatua inayozalisha fahari ya kweli ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, uwekezaji katika kizimba kimoja una uwezo wa kuzalisha hadi tani 3.5 za samaki, jambo linalomhakikishia kijana faida ya zaidi ya Sh milioni tisa ndani ya miezi saba, huu ukiwa ni ushahidi wa mapinduzi ya dhati ya kipato.
Ufanisi wa mradi huu unajidhihirisha zaidi kupitia nidhamu ya urejeshaji wa mikopo, ambapo tayari Sh bilioni 2.1 zimesharejeshwa na kuanza kuzungushwa kwa wanufaika wengine wapya nchini.
Mwakilishi wa TADB amebainisha kuwa zaidi ya Sh bilioni 14 zimekwishatolewa bila riba ndani ya miaka miwili ili kuimarisha sekta hiyo, jambo linaloimarisha imani ya jumuiya ya kimataifa na wadau wa maendeleo kwa Tanzania. Licha ya changamoto ndogo za usambazaji wa vifaa, mafanikio ya vijana hawa kufika hadi masoko ya Afrika Mashariki ni ishara tosha kuwa Tanzania inaaminika, inajulikana, na vijana wake sasa wako tayari kuandika historia mpya ya mafanikio kupitia uchumi wa bluu.

Post a Comment