WIZARA YA AFYA YATAHADHARISHA ONGEZEKO LA MAFUA MAKALI, COVID-19 NA DENGUE
WIZARA ya Afya imetoa tahadhari kwa umma kufuatia ripoti ya ufuatiliaji wa mwenendo wa magonjwa ya mlipuko kuonesha ongezeko la wagonjwa wa mafua makali (Influenza) na Covid-19 nchini. Ongezeko hilo linatajwa kwenda sambamba na msimu wa kuanzia mwezi Novemba hadi Aprili, ambapo takwimu za kidunia huonesha kupanda kwa maambukizi ya magonjwa hayo ya mfumo wa hewa.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amebainisha kuwa magonjwa haya huenea kwa kasi kupitia majimaji kutoka kwenye njia ya hewa wakati mtu mwenye maambukizi anapopiga chafya, kukohoa au kuzungumza. Aidha, maambukizi yanaweza kusambazwa kwa kugusa mazingira au vifaa vilivyochafuliwa na majimaji hayo.
Dalili na Tahadhari ya Influenza na Covid-19
Dkt. Magembe amewataka wananchi kuwa makini na dalili kama homa kali, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu usio wa kawaida. Ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi hayo, Wizara imehimiza hatua zifuatazo:
Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Kuepuka misongamano isiyo ya lazima au kuvaa barakoa unapokuwa kwenye maeneo yenye watu wengi.
Kuwahi kituo cha afya na kuepuka matumizi ya dawa (antibayotiki) bila ushauri wa kitaalamu.
Tishio la Homa ya Dengue
Sambamba na magonjwa ya hewa, Dkt. Magembe ametoa tahadhari ya ugonjwa wa Homa ya Dengue kutokana na kuingia kwa msimu wa mvua za masika zinazosababisha kuongezeka kwa mazalia ya mbu. Ugonjwa huu huenezwa na mbu aina ya Aedes (mbu mweusi mwenye madoa meupe) ambaye huuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni.
Wizara imetoa rai kwa jamii kutokomeza mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi, kuharibu makopo yaliyotupwa, matairi ya zamani na vifuu. Wananchi wanahimizwa kuvaa nguo ndefu, kuweka nyavu kwenye madirisha na kuwahi matibabu wanapoona dalili zinazofanana na malaria kama homa kali na maumivu ya macho.
Hali ya Kipindupindu Nchini
Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Serikali ameshukuru wadau mbalimbali, ikiwemo WHO, taasisi za dini na vyombo vya habari, kwa jitihada zilizosaidia kudhibiti mlipuko wa kipindupindu. Ingawa kwa mwezi mmoja uliopita hakuna mkoa ulioripoti kisa kipya cha kipindupindu (ukiondoa Kilimanjaro na Njombe ambazo awali hazikuathirika), Dkt. Magembe amesisitiza kuwa nchi bado ipo katika hatari, hivyo usafi wa mazingira na maji lazima uendelee kuzingatiwa kikamilifu.

Post a Comment