TRA YAMWAGA MAMILIONI KWA WABUNIFU; KUNA MTU KALAMBA MILIONI 50
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa tuzo kwa washindi wa shindano la ubunifu lengo likiwa ni kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato na kurahisisha utoaji huduma kwa walipakodi nchini. Katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya TRA jijini Dar es Salaam, jumla ya wabunifu kumi walizawadiwa mamilioni ya fedha, ngao, na vyeti vya heshima.
Bwana Gabriel Mashenene ameibuka mshindi wa kwanza baada ya kupata wastani wa alama 92%, akijinyakulia kitita cha shilingi milioni 50 taslimu. Mashenene amebuni mfumo wa kidijitali uitwao 'KodiTrack' unaolenga kupambana na ankara bandia na udanganyifu wa uagizaji bidhaa kwa kufanya uhakiki wa taarifa za mizigo kwa wakati halisi (real-time).
Washindi wengine waliofuatia ni Edmund Komba, Emma Sambaya, na Malehe Masubi ambao kila mmoja amezawadiwa shilingi milioni 30. Ubunifu wa Komba unahusu matumizi ya QR Code na GPS kufuatilia bidhaa bandia, huku Emma Sambaya akipendekeza kuunganishwa kwa risiti za EFD na mfumo wa bima ya afya (NHIF) ili kumuwezesha mlipakodi kuchangia bima kupitia sehemu ya VAT. Kwa upande wake, Malehe Masubi amebuni mfumo wa kutumia Akili Mnemba (AI) kurahisisha kazi za kiofisi.
Aidha, kundi la washindi wengine sita likiongozwa na Ng’wang’wa Loyani, Erick Joachim, Ajra Noordin Ismail, Hubayb Said, Ismael Mkumbi, na Erick Joachim (mshindi wa mara mbili katika kundi hili) walizawadiwa shilingi milioni 20 kila mmoja kwa mawazo yao ya kidijitali yanayolenga kuimarisha ufuataji wa sheria za kodi na matumizi ya teknolojia ya Blockchain.
Akizungumza katika hafla hiyo, uongozi wa TRA umesisitiza kuwa taasisi isiyokumbatia ubunifu hupitwa na wakati, hivyo mamlaka hiyo itaendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Post a Comment