Serengeti Boys dhidi ya Senegal AFCON, Samia Atoa Baraka zote




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Timu ya Taifa ya Vijana chini ya Umri wa Miaka 17, Serengeti Boys, kwa kufuzu kucheza mchezo wa fainali ya michuano ya mpira wa miguu barani Afrika kwa vijana ya AFCON U17 nchini Morocco.

Aidhja ametoa pongezi pia kwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar mwezi Novemba, 2026. 

Mheshimiwa Rais ameyataja mafanikio hayo kuwa ni hatua muhimu kwa maendeleo ya soka la vijana nchini yanayoakisi vipaji, juhudi, na nidhamu ya vijana wa Tanzania katika uwakilishi wa kimataifa.

Kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari S. Machumu, Rais amewatakia Serengeti Boys kila la kheri katika mchezo huo wa fainali utakaofanyika Jumanne ijayo ya tarehe 02 Juni, 2026 dhidi ya Senegal, akieleza imani yake kubwa kuwa wataendelea kuonesha kiwango bora na kuitangaza vyema nchi.

Hatua hii ya kihistoria inafuatia ushindi wa kukata na shoka ambapo Tanzania na Senegal zilifanikiwa kutinga fainali baada ya kushinda mechi za nusu fainali zilizokuwa na upinzani mkali na kuamuliwa kwa matuta mjini Rabat. 

Serengeti Boys ilitinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yao kwa kuiondosha Misri kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana, wakati wapinzani wao Senegal wakiwaondosha wenyeji Morocco kwa penalti 7-6 baada ya sare ya bao 1-1. 

Fainali hii inatarajiwa kuwa ya kusisimua sana ikizikutanisha Tanzania, ambayo imepeleka mshangao mkubwa na kuwa gumzo la mashindano, dhidi ya Senegal wenye sifa inayokua ya kuwa moja ya mataifa yenye nguvu zaidi katika soka la vijana barani Afrika. Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Moulay El Hassan mjini Rabat saa mbili usiku kwa saa za huko.

Safari ya Serengeti Boys kuelekea fainali imekuwa moja ya hadithi za kuvutia zaidi katika mashindano haya, kwani mchezo wao dhidi ya Misri ulikuwa wa mbinu nyingi na mgumu, huku timu zote zikipata tabu kutengeneza nafasi za wazi.

Misri walikaribia kupata bao mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Daniel Tamer, lakini shuti lake kali liliokolewa vyema na kipa wa Tanzania, Haji Abdallah. 

Baada ya dakika 90 kukamilika bila timu hizo kufungana, vijana wa Tanzania walionesha utulivu mkubwa kwenye hatua ya matuta na kufunga penalti nne kati ya tano, jambo lililohitimisha ushindi wao wa kihistoria na kuzima ndoto za Misri waliokuwa wametinga nusu fainali yao ya kwanza tangu mwaka 2003, ingawa nao wamefuzu Kombe la Dunia.

Kwa upande wa Senegal, njia yao ya kuelekea fainali ilikuwa ya vitendo zaidi pale walipowaondosha wenyeji Morocco mbele ya mashabiki wao wengi waliokuwa na shauku kubwa. 

Simba Vijana wa Teranga walitangulia kupata bao katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Mouhamed Wagne, aliyewahi mpira uliookolewa na kipa wa Morocco, Rayan Yaakoubi, kufuatia shuti la Souleymane Commissaire Faye.

Morocco walipambana sana kusawazisha na walifanikiwa katika dakika za nyongeza za mchezo kupitia kwa Ismail El Aoud aliyefunga mpira uliorudi baada ya penalti yake ya awali kuokolewa na kipa wa Senegal, Assane Sarr. Katika hatua ya matuta, kipa Sarr aliibuka shujaa wa Senegal na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa penalti 7-6.

Kabla ya kushuhudia fainali hiyo kubwa, wenyeji Morocco watachuana na Misri katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu utakaopigwa Jumatatu ya tarehe 01 Juni, 2026 katika uwanja wa CMVI-T8 saa mbili usiku kwa saa za huko. 

Mchezo huo unatoa fursa kwa timu zote mbili kumaliza mashindano kwa ushindi baada ya masikitiko ya nusu fainali. Baada ya mashindano yaliyojaa mabao, mambo ya kushangaza na msisimko wa changamoto za penalti, fainali ya michuano hii sasa itahitimishwa kwa Tanzania na Senegal kupigania taji la bara, ambapo kwa Tanzania inawakilisha fursa ya kipekee ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa AFCON U17, huku Senegal wakitaka kudhihirisha hadhi yao kama wazalishaji wakuu wa vipaji vya soka la vijana barani Afrika.

No comments