KIKWETE AELEZA UHUSIANO WAKE NA KARDINALI PENGO




RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo amefichua historia ya muda mrefu ya urafiki na ushirikiano uliokuwepo kati yake na aliyekuwa Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Dkt. Kikwete ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuweka saini katika kitabu cha maombolezo kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, kufuatia kifo cha kiongozi huyo wa kiroho kilichotokea tarehe 19 Februari, 2026.

Uhusiano wa Kikazi na Kiurafiki

Akizungumza na waandishi wa habari kwa majonzi, Dkt. Kikwete ameeleza kuwa urafiki wao una mizizi ya tangu miaka ya mapema ya utumishi wao kwa umma. Alikumbusha kuwa alifahamiana na Kardinali Pengo wakati yeye akihudumu wilayani Nachingwea mkoani Lindi, ikiwa ni kituo chake cha kwanza cha kazi.

Wakati huo, Marehemu Kardinali Pengo alikuwa akihudumu kama Askofu aliyesimamia maeneo ya Tunduru na Lindi (Nachingwea ikiwa ndani yake). Dkt. Kikwete amemtaja marehemu kama kiongozi aliyekuwa na upendo wa dhati kwa watu wote na aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika ustawi wa kijamii na kiroho.

"Marehemu Kardinali Pengo atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa kwa Kanisa na Taifa. Alikuwa rafiki wa wengi na kiongozi aliyegusa maisha ya watu wengi kupitia huduma yake ya kiroho na kijamii," alisema Dkt. Kikwete.

Rambirambi kwa Kanisa




Baada ya zoezi la kuweka saini, Dkt. Kikwete alimpa mkono wa pole Askofu Mkuu wa sasa wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Thaddaeus S. Ruwa’ichi. Alitoa pole kwa viongozi wote wa Kanisa Katoliki, watawa, na waumini, akiwataka kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu huku akiungana nao kumuombea marehemu apumzike kwa amani.

Ratiba ya Mazishi

Kwa mujibu wa utaratibu uliotangazwa, waombolezaji watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho siku ya Jumamosi, tarehe 28 Februari 2026, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu kuanzia saa 03:15 asubuhi.

Siku ya Jumapili, tarehe 1 Machi 2026, mwili utasafirishwa kuelekea Kituo cha Hija Pugu kwa ajili ya Misa ya Mazishi itakayofanyika saa 04:00 asubuhi, na kuhitimishwa na maziko katika eneo hilo hilo la Pugu.

Marehemu Kardinali Pengo, aliyetawazwa kuwa Kardinali mwaka 1998, anakumbukwa kama mwanateolojia mbobezi na sauti ya busara iliyoshiriki katika mikutano mikubwa ya kimataifa, ikiwemo ile ya kumchagua Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani (Papa) mwaka 2005 na 2013.Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 na kupadrishwa mwaka 1971.

Alisoma Teolojia ya Maadili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran mjini Roma, ambako alipata shahada ya uzamivu mwaka 1977. Baadaye alifundisha katika Seminari ya Kipalapala na kuwa gombera wa kwanza wa Seminari ya Segerea hadi mwaka 1983.

Aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea mwaka 1983 na baadaye Askofu wa Jimbo la Tunduru–Masasi mwaka 1985. Mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu Msaidizi wa Dar es Salaam na mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu kamili wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mwaka 1998 alitangazwa kuwa Kardinali na Papa Yohane Paulo II, na alishiriki katika mikutano ya kumchagua Papa mwaka 2005 na 2013.

Kardinali Pengo alihudumu pia katika idara mbalimbali za Kanisa Katoliki la Roma na kuongoza Baraza la Makanisa Katoliki Afrika (SECAM) tangu mwaka 2007. Alistaafu mwaka 2019, akiacha alama ya uongozi thabiti na imani isiyotetereka.


No comments