VIJANA WATAMBUA MTAJI PEKEE WA KUJENGA TANZANIA YA KESHO
Kama Taifa, tunapaswa kuhubiri upendo na mshikamano. Maendeleo hayaji kwa kelele za vurugu, bali huja kwa vitendo vya ushirikiano. Kijana, chagua kuwa mlinzi wa amani ya mtaa wako, kijiji chako, na nchi yako. Kumbuka, amani ikitoweka, sote tunakuwa wakimbizi katika nchi yetu wenyewe.
Katika ulimwengu wa sasa unaokwenda kasi, vijana ndio injini ya mabadiliko na nguvu kazi ya Taifa. Hata hivyo, nguvu hiyo haina maana kama itatumika katika vurugu au mifarakano. Tunapaswa kuelewa kuwa vurugu hazijawahi kuleta mkate mezani; badala yake, huacha makovu ya umaskini, dhiki, na majuto. Ili tusonge mbele, ni lazima tuchague njia ya busara—njia ya amani.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya ya Mkuranga, Shukuru Ngweshani, anatukumbusha kuwa msingi wa amani ni kuaminiana bila kubaguana. Tunapokubali kukaa pamoja na kufanya kazi kama timu moja, tunafungua milango ya maendeleo ambayo hakuna vurugu inayoweza kuifungua. Utulivu na mshikamano si maneno tu ya kisiasa, bali ndiyo jadi na utambulisho wa nchi yetu tangu asili. Tukishirikiana, tunashinda; tukibaguana, tunapoteza sote.
Amani si jambo la kuchukulia poa; ni ngao yetu kuu kama anavyosema Mkurugenzi wa African Talent Forum (ATF), Rosemary Bujashi. Mkurugenzi huyu anasisitiza kuwa lazima kuilinda amani kwa gharama yoyote ili kujilinda na wale wasioitakia mema nchi.
Ukiingia mitandaoni unaona kuna watu na makundi yanayofurahia kuona jamii ikigawanyika kwa sababu katika mgawanyiko huo, wao wanapata mwanya wa kurudisha nyuma maendeleo kwa kuwa mawakala wa uharibifu. Kuilinda amani ni kulinda mustakabali wa maisha yetu, elimu yetu, na biashara zetu.
Vijana mara nyingi ndio hulengwa kutumika katika makundi yanayoyumbisha nchi kiuchumi na kijamii. Diwani wa Kata ya Mkuranga, Hamza Mahanaka, anatoa wito mahususi kwa vijana kuachana na makundi yanayorudisha nyuma juhudi za maendeleo kwani hakuna mwekezaji atakayeweka fedha zake mahali penye hofu.
Pia amani inaruhusu mama ntilie, mkulima, na kijana wa bodaboda kufanya kazi masaa 24 bila hofu hivyo kuwawezesha kupata kipato cha kuhudumia kaya zao na kulipa kodi kwa ya maendeleo ya taifa.
Post a Comment