UTULIVU UNYOVYOSAFISHA NJIA YA MAFANIKIO KWA VIJANA



Katika kuelekea kuimarisha misingi ya taifa letu, sauti za wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini zimeendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu kama nguzo kuu ya maendeleo na umoja wa kitaifa. 

Mkazi wa Mtaa wa Visegese katika Kata ya Chamwino mkoani Morogoro, Mary Makoa, anatoa wito wa dhati kwa vijana wa Kitanzania kuwa wazalendo na wenye bidii katika kudumisha amani ili waweze kurithi taifa lenye utulivu pindi watakapokuwa viongozi wa baadaye. 

Amewataka vijana kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani ambayo imejengwa kwa miongo mingi na waasisi wa taifa hili, akiamini kuwa uzalendo ndio msingi wa uongozi bora.

Hali kadhalika, umuhimu wa kujitafakari kama Taifa umesisitizwa na Daudi Inuka, mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, ambaye anahimiza kila Mtanzania kuona thamani ya umoja na mshikamano tulionao. Inuka anabainisha kuwa amani inapotoweka, maisha ya mwanadamu hubadilika ghafla na kuingia katika taharuki kubwa inayovuruga mfumo mzima wa maisha na maendeleo. Ni wazi kuwa amani si jambo la kuchukulia mzaha, bali ni tunu inayopaswa kulindwa kwa nguvu zote na kila mwananchi ili kuepuka majanga yanayoweza kulikumba taifa endapo utulivu utatoweka.

Kwa upande wake, Musa Mseti ambaye pia ni mkazi wa Bariadi, anafafanua kuwa amani ndiyo kiini cha kila kitu tunachokiona kikifanikiwa nchini, kwani shughuli zote za kijamii na kiuchumi zinawezekana tu pale ambapo kuna utulivu. Akigusia matukio ya nyuma yaliyoleta hofu, Mseti anabainisha kuwa kuwepo kwa amani kuna maana kubwa sana kwa sababu sote tumeshuhudia jinsi taharuki inavyoweza kuvuruga utulivu wa nafsi na jamii kwa ujumla. Hivyo basi, simulizi hizi za wananchi zinatukumbusha kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila mmoja wetu, tukianzia na vijana ambao ndio walinzi wa urithi wa kesho wa taifa letu.

No comments