MFUMO WA MO DEWJI WAGUSWA: KATIBA MPYA YA SIMBA SASA YARUHUSU WAWEKEZAJI 'KIBWENE'
KLABU ya Simba sasa imeingia rasmi
katika mfumo mpya wa uendeshaji kufuatia Serikali, kupitia Baraza la Michezo la
Taifa (BMT), kuidhinisha marekebisho ya katiba ya klabu hiyo ambayo sasa
yanaruhusu wawekezaji zaidi ya mmoja kumiliki hisa ndani ya wekundu hao wa
Msimbazi.
Hatua hiyo imekuja baada ya mchakato
mrefu wa kisheria kukamilika kwa Msajili wa Vyama vya Michezo, ikiwa ni
utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul
Makonda, aliyetaka suala hilo kuhitimishwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Mapinduzi
ya Umiliki: Hisa 49 kwa 51
Katika katiba hiyo iliyofanyiwa
maboresho, Simba sasa inafungua milango kwa wawekezaji mbalimbali kugombea
asilimia 49 ya hisa za klabu, huku asilimia 51 zikibaki mikononi mwa Baraza la
Wadhamini kwa niaba ya wanachama.
Mabadiliko hayo yanalenga kuiondoa
Simba katika utegemezi wa mwekezaji mmoja na badala yake kuleta mtaji mpana
zaidi utakaoweza kuhimili ushindani wa soka la kisasa ndani na nje ya nchi.
Muundo
wa Kampuni na Usimamizi wa Mali
Moja ya mambo mazito yaliyomo kwenye
katiba hiyo ni kutambuliwa rasmi kwa kampuni ya Simba Sports Club Company
Limited. Chombo hiki ndicho kitakachokuwa na jukumu la kusimamia masuala
yote ya kibiashara na kiutendaji ya klabu.
Pia, Baraza la Wadhamini limepewa
meno zaidi, ambapo litakuwa na wajumbe kati ya watano na saba wenye jukumu la
kulinda mali za klabu. Msajili wa Vyama vya Michezo, Abel Ngilungwa,
amebainisha kuwa maboresho hayo yamezingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) uliotolewa Mei 12, 2025.
📦 BOKSI: MAMBO 4 MAKUBWA KATIBA MPYA YA SIMBA
- Wawekezaji Zaidi ya Mmoja: Sasa Simba si ya mtu mmoja; asilimia 49 ya hisa ziko
wazi kwa wawekezaji wengi.
- Umiliki wa Wanachama:
Wanachama wanabaki na asilimia 51 kupitia Baraza la Wadhamini.
- Chombo cha Biashara:
Simba Sports Club Company Limited ndiyo 'injini' ya fedha na utendaji.
- Ulinzi wa Mali:
Baraza la Wadhamini (Wajumbe 5-7) ndilo mlinzi mkuu wa mali zote za Simba.
Kauli
ya Msajili
Akizungumza jana Februari 18, 2026
wakati akikabidhi rasmi katiba hiyo kwa uongozi wa Simba, Ngilungwa alisema
marekebisho hayo hayalengi kuleta migogoro bali kuimarisha utawala bora.
"Mchakato huu umepitia
uchambuzi wa kina ili kuhakikisha katiba inabeba madhumuni yaliyokusudiwa.
Tayari uongozi wa Simba umeshasaini kuthibitisha kukubaliana na yaliyomo, na
sasa mchakato huu uliokuwa unasubiriwa kwa hamu umehimitishwa rasmi," alisema Ngilungwa.
Agizo
la Makonda Litekelezwa
Kukamilika kwa mchakato huu kumekuja
siku mbili tu tangu Waziri Paul Makonda kutoa shinikizo kwa ofisi ya Msajili.
Maboresho haya yanatajwa kuwa yatasaidia Simba kuendeshwa kwa uwazi zaidi na
kutoa mazingira rafiki kwa wadau wengine wa biashara kujitokeza kuwekeza klabuni
hapo.
Kwa hatua hii, Simba sasa
inasubiriwa kuitisha Mkutano Mkuu au kutoa mwongozo wa namna gani wawekezaji
hao wapya wataingia sokoni, huku Mkutano Mkuu ukibaki kuwa chombo chenye
mamlaka ya mwisho ya maamuzi.

Post a Comment