NDOTO YA VIJANA NA MUSTAKABALI WA TAIFA: TAFSIRI YA BAJETI MPYA KATIKA KUIFUNGUA NCHI
Katika kumbi za Bunge jijini Dodoma, kumesikika sauti ya matumaini inayobeba mustakabali wa mamilioni ya Watanzania, hususan vijana wanaosubiri kwa hamu kuona milango ya fursa ikifunguka.
Hatua ya Serikali kuwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Shilingi trilioni 61.934 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 si tu suala la namba na takwimu za kifedha, bali ni mwelekeo mpya wa namna nchi inavyojipanga kuwakomboa vijana wake na kuwapa nafasi ya kujidai ndani ya uchumi wa kisasa.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameweka wazi kuwa serikali imejipanga kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika rasilimali watu, jambo ambalo ndilo mzizi wa ajira na maendeleo ya kijamii.
Kupitia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kipaumbele kimeelekezwa katika kujenga uchumi shindani na jumuishi. Hii ina maana kuwa serikali inatengeneza mazingira ambapo kijana wa Kitanzania hatakuwa mtazamaji tu, bali mshiriki mkuu katika miradi ya kielelezo na kimkakati inayotekelezwa kote nchini.
Kufunguliwa kwa nchi kupitia bajeti hii kunaonekana wazi katika ongezeko la matumizi yanayolenga kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali.
Serikali inapowekeza zaidi ya nusu ya bajeti yake katika ruzuku kwa taasisi, mashirika ya umma, na mamlaka za mitaa, inatengeneza mnyororo mrefu wa thamani ambao mwisho wa siku unazalisha ajira kwa vijana wa kada mbalimbali. Ni mpango unaolenga kumpa kijana uhakika wa maisha kupitia ujuzi wake, huku ukiongeza thamani ya nguvu kazi ya taifa ili iweze kushindana hata katika soko la kimataifa.
Zaidi ya ajira na uchumi, bajeti hii imebeba dhamana ya kulinda amani na utulivu wa taifa. Amani ya kweli inategemea matumaini ya wananchi wake, na serikali imeliona hilo kwa kuelekeza fedha nyingi katika huduma za jamii na kuimarisha misingi ya uendelevu.
Kijana mwenye uhakika wa kipato na fursa hana sababu ya kukata tamaa, badala yake anakuwa mlinzi wa amani na mjenzi wa taifa lake. Hii ndiyo tafsiri halisi ya kuifungua nchi, ambapo uhuru wa kiuchumi unakuwa kichocheo cha utulivu wa kijamii.
Mwelekeo wa muda wa kati hadi mwaka 2029 unaonyesha kuwa Tanzania ipo katika mapinduzi makubwa ya kifikra na kiutekelezaji.
Kwa kuweka msisitizo katika kukua kwa mapato ya ndani na kupunguza utegemezi, nchi inajenga uwezo wa kujiamulia hatma yake. Hili ni jambo la kujivunia kwa vijana, kwani linafungua milango ya ubunifu na uwekezaji ambayo hapo awali ilionekana kuwa na vikwazo. Kwa bajeti hii, serikali haitoi tu fedha, bali inatoa dira ya wapi nchi inaelekea na jinsi gani kila raia anaweza kunufaika.
Tunapoelekea kwenye utekelezaji wa bajeti hii, matarajio ni kuona mabadiliko ya kweli mitaani na vijijini. Ni wakati wa vijana kuchamka na kuchangamkia fursa zitakazotokana na ufunguzi huu wa nchi. Msingi uliowekwa na Balozi Omar bungeni ni mwanzo wa safari ndefu ya kuelekea Tanzania yenye neema, ambapo amani itastawi kupitia kazi, na vijana wataweza kutembea kifua mbele wakijidai kwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya ardhi yao.

Post a Comment