AMANI NA MATUMAINI YETU INAVUTIA DUNIA KUFURIKA KUJIFUNZA KILIMO



Katika hali inayodhihirisha kuwa Tanzania ni kitovu cha utulivu na chemchemi ya maarifa barani Afrika, jiji la Dar es Salaam linajiandaa kuandika historia nyingine kwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa zana endelevu za kilimo barani Afrika.

Mkutano huu utakaowakutanisha wadau wa kimataifa na viongozi wa juu wakiongozwa na Waziri Mkuu Daktari Mwigulu Nchemba unathibitisha kuwa dunia imeweka imani yake yote kwa nchi yetu kama sehemu salama na yenye utulivu wa kipekee kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kimkakati ya kuwakwamua wananchi kiuchumi na kuleta mageuzi ya kijani kupitia teknolojia za kisasa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amepaza sauti na kubainisha kuwa ugeni huu mkubwa unaofanyika kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ni fursa ya dhahabu kwa vijana na taifa kwa ujumla kubadilishana uzoefu na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.

Mwakilishi wa shirika hilo Charles Tulai akisisitiza kuwa nguvu ya vijana ndiyo injini itakayozima changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu.

Tunapowakaribisha wageni hawa kutoka kila pembe ya Afrika tunafanya hivyo kwa kifua mbele tukijua kuwa Tanzania siyo tu kisiwa cha amani bali ni shule ya vitendo ambapo ubunifu wa kijana wa kijijini na mikutano mikubwa ya kimataifa vinakutana ili kuimarisha uchumi wa taifa na kumpa kila mwananchi nafasi ya kunufaika na rasilimali zetu .

No comments