KIPAJI NA JUHUDI NI DHAHABU KUU KULIKO VYETI VYA MAKARATASI, SOMO KUTOKA WANGING'OMBE




Mbunifu  Eston Chaula kutoka ardhi ya baraka ya Wanging’ombe mkoani Njombe  amethibitisha kuwa akili na kipaji ni zawadi ya asili inayohitaji juhudi na uthubutu kuliko hata makaratasi ya shule kwani kijana huyu mwenye elimu ya msingi pekee ameweza kuishangaza jamii kwa kutengeneza mashine na zana zinazorahisisha kazi za kilimo na ujenzi.

Na amefanya yote hayo bila hata kukanyaga mlango wa chuo chochote cha ufundi wala kusoma teknolojia kutoka kwa maprofesa hali inayotupa picha kuwa uwezo wa binadamu haupimwi kwa vyeti bali kwa matunda ya mikono yake na jinsi anavyoweza kuwa msaada kwa watu wanaomzunguka.

Inasisimua kuona namna kijana huyu alivyogeuka kuwa mkufunzi anayewaongoza vijana wenzake na hata watu waliomzidi elimu wakisafiri umbali mrefu kutoka nje ya mkoa wa Njombe ili kupata maarifa kutoka kwake jambo ambalo ni kielelezo tosha kuwa dunia ya sasa inahitaji watu wenye majibu ya matatizo ya jamii na siyo tu watu wenye sifa za kitaaluma zisizo na tija.

Uwajibikaji wa kijana huyu umeenda kinyume na wasomi wengi walioishia kujisifia kwa maandishi na idadi ya makaratasi bila kuvumbua kitu chenye mguso wa moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida huyu mwamba wa Wanging’ombe anatoa darasa la vitendo namna ya kuachana na jembe la mkono na kuleta mabadiliko ya kweli katika uzalishaji kupitia mashine zinazookoa muda na nguvu kazi

Ujumbe kwa vijana wote ni kwamba wakati wa kulalamika umepitwa  na badala yake kila mmoja anapaswa kuamsha kipaji kilicholala ndani yake kwa kutumia mazingira yanayomzunguka kujifunza na kuthubutu kufanya mambo makubwa kama anavyofanya Eston Chaula ambaye leo hii anaitwa injinia wa vitendo akiziba pengo la wataalamu wenye shahada ambao wakati mwingine wamebaki kuwa wasaini mikataba. 

Siri ya mafanikio ya kijana huyu wa Njombe imejifichika kwenye utayari wake wa kutatua kero za wakulima na mafundi wenzake jambo ambalo ni mwarobaini wa ukosefu wa ajira kwa kuwa yeye hajakaa kusubiri kuajiriwa bali amejiajiri na sasa anaajiri wengine kwa kuwapa ujuzi na moyo wa kupambana bila kukata tamaa.

No comments