ACHANENI NA UVUMI ,CAF YATHIBITISHA AFCON 2027 KUFANYIKA TANZANIA, KENYA NA UGANDA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limethibitisha kuwa michuano ya Mataifa ya Afrika, Africa Cup of Nations, itafanyika katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 13, 2026 katika ukumbi wa hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Rais wa CAF, Patrice Motsepe, amesema uvumi unaosambazwa mitandaoni kuwa mataifa hayo hayako tayari kuandaa mashindano hayo hauna ukweli.
Amesisitiza kuwa AFCON 2027 itakuwa na mafanikio makubwa zaidi katika historia, akieleza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri. Aidha, amesema Tanzania, Kenya na Uganda zilijipambanua vyema katika michuano ya African Nations Championship (CHAN), hivyo hakuna sababu ya kupokonywa uenyeji huo.
“Nina imani na mataifa haya na ninajivunia kazi inayofanywa na viongozi wa mpira wa miguu katika mataifa haya matatu,” amesema Dkt. Motsepe.
Aidha, amewataka viongozi kuendelea kuboresha miundombinu ili kuhakikisha mashindano yanafanyika bila kasoro.
Rais huyo aliwasili rasmi nchini Tanzania asubuhi ya leo kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Kamati Tendaji ya Shirikisho hilo na kupokelewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Makonda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere International Airport, Terminal 1, jijini Dar es Salaam.

Post a Comment