TUME YA UCHUNGUZI WA VURUGU ZA UCHAGUZI YAZUNGUMZA NA MAHABUSU GEREZA KUU ARUSHA,
Tume
ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, imetembelea Gereza Kuu la Arusha kusikiliza
ushahidi wa makundi mbalimbali.
Akiwa
gerezani hapo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman
Chande, amefanya mazungumzo na uongozi wa gereza pamoja na mahabusu 10
waliosalia gerezani humo kutokana na matukio hayo.
Mahabusu hao,
wakiwemo wanaume kenda (9) na mwanamke mmoja (1), wanatarajiwa kufikishwa
mahakamani tena Januari 14, 2026.
Jaji
Mstaafu Chande amebainisha kuwa lengo la tume hiyo ni kuzungumza na wahusika na
waathirika wa makundi yote ili kubaini kiini cha machafuko hayo na kutoa
mapendekezo yatakayozuia matukio kama hayo kujirudia katika mustakabali wa
Taifa.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Gereza Kuu Arusha, Vicent Karani, ameitaarifu tume hiyo
kuwa awali walipokea jumla ya mahabusu 197 waliohusishwa na vurugu za uchaguzi.
Hata hivyo, mahabusu 187 tayari wameachiwa huru na mahakama, huku 10 waliosalia
wakikabiliwa na kosa la pili la nyongeza.
Tume
hiyo inaendelea na ziara zake katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya kuhoji
waathirika na kukusanya taarifa kamili kabla ya kuwasilisha ripoti rasmi kwa
mamlaka husika.
Post a Comment