Mambo matano kuzingatiwa kujenga umahiri KKK
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itazingatia mambo matano katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa mpango huo unawaolenga wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza na darasa la pili. Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.
Profesa Mkenda alisema jambo la kwanza watahakikisha wanaimarisha namna ya ufundishaji kwa kufanya mafunzo endelevu kwa walimu na kusimamia namna ya bora ya kufundisha elimu ya awali, darasa la kwanza na la pili.
Alisema jambo la pili watasimamia maendeleo endelevu ya walimu kwa kuwaandaa, kuwashirikisha hasa katika kuandaa vifaa vya kufundishia pamoja na kuwa na nyenzo za kufundishia na kujifunzia zinazopatikana kote nchini.
Alisema jambo la tatu ni kuwa na nyenzo za kufundishia na kujifunzia ambazo nyingi zinapatikana katika mazingira ya Tanzania.
Profesa Mkenda alisema jambo la nne watahakikisha wizara hiyo inafanya upimaji kama sehemu ya sayansi ili ndani ya miaka nane wawe wamewatengenezea uwezo wanafunzi ili kuhakikisha wanafanya vizuri.
Aidha, alisema watahakikisha wanafanya tathmini na upimaji pamoja na kuhakikisha wanafanya ushirikishwaji wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili kuongeza kasi ya uwezo wa wanafunzi.
“Baada ya ufunguzi tutakuwa tunatekeleza, tutasimamia na tutafuatiliana maendeleo ya mkakati huu kwa kushirikiana na Ofisi wa Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na tutajitahidi kila mwaka tuwe tunakupa mrejesho wa maendeleo ya utekelezaji wa mpango mkakati huu ambao utekelezaji wake utachukua hadi miaka mitano mpaka 2031,’’ alisema Profesa Mkenda mbele ya Rais Samia.
Alisema uzinduzi wa KKK umeonesha namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza ahadi ambazo Rais Samia aliahidi Agosti 28, 2025 wakati wa ufunguzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Wakati ukifungua kampeni uliahidi kwamba ndani ya siku 100 za kwanza serikali yako itakuja na mpango mkakati wa kisayansi wa kukuza masuala ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, leo serikali yako imetimiza yale uliyoyaahidi na siku 100 zikiwa bado hazijatimia,” alisema Profesa Mkenda.

Post a Comment