TCRA YAPITIA UPYA MFUMO WA KISHERIA WA USIMAMIZI WA SEKTA YA POSTA




MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapitia upya mfumo wa kisheria na usimamizi wa sekta ya posta ili kuwezesha uanzishwaji wa aina mpya za biashara.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amesema  hatua hiyo inakwenda sambamba na kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya ubora wa huduma na kuhakikisha uendelevu wa sekta kwa  muda mrefu.

Dk Bakari alisema Dar es Salaam  kwamba TCRA inatambua ukuaji endelevu wa shughuli za posta na usafirishaji vifurushi unatakiwa kuimarishwa na kanuni imara zinazozingatia  masuala ya jamii, mazingira na utawala.  

“Kujumuisha masuala haya katika mfumo wa usimamizi ni muhimu ili kuhakikisha kuwa sekta inaendelea kuwa stahimilivu, jumuishi na inayokabiliana na changamoto zinazojitokeza kwenye teknolojia, uchumi na mazingira” alisema hivi karibuni.

Dk Bakari ameielezea sekta ya posta kama mwezeshaji wa uchumi wa kidijiti Afrika kupitia matumizi ya tehama kutokana  na nafasi yake kwenye kufanikisha biashara mtandao. 

“Kadri biashara ya mtandaoni inavyoendelea kupanuka, sekta ya posta ina majukumu muhimu katika kuunganisha biashara na watumiaji, kuwezesha biashara mipakani na kuhakikisha kuwa  vitu vya posta vinafikishwa kwa uhakika kwa wenyewe, hasa walioko vijijini na jamii kwenye maeneo yasiyofikiwa na huduma kikamilifu,”alisema Dk Bakari.

Aidha, alisema sekta inaendelea kubaki kwenye nafasi ya kipekee ya kuwezesha ukuaji jumuishi kwa kuunganisha watu, biashara na masoko. 

“Ubia wa kimkakati wa taasisi za serikali, kampuni binafsi zinazotoa huduma za usafirishaji vifurushi, mifumo ya kidijitali na washirika wa maendeleo, sekta ya posta vinaweza kufungua fursa mpya kwa biashara ndogo na za kati, kuboresha uvumbuzi, na kuwezesha ukuaji wa uchumi wa kidijitali,”alisema Dk Bakari.

Alisema pamoja na changamoto zilizojitokeza, huduma za posta bado ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.  

Dk Bakari alisema TCRA inaendeleza utunzaji wa mazingira kwa kuhimiza matumizi bora ya njia za kusafirisha vifaa na kutumia  vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati kwa ufanisi na ambavyo  havitoi hewa chafu. Vilevile inaweka kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za posta kwa wote. 

Alisisitiza dhamira ya TCRA kuendeleza ushirikiano wa kikanda na uzingatiaji wa masuala ya pamoja kwenye usimamizi kupitia taasisi za kikanda na kimataifa zinazojihusisha na mawasiliano. Hizo ni pamoja na PAPU, Umoja wa  Mawasiliano  Afrika Mashariki (EACO) na Chama cha Wasimamizi wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA). 

Alisema ushirikiano huo unawezesha kushinda changamoto zilizoko kipindi hiki na kujenga dunia ambapo ubadilishanaji wa bidhaa na taarifa hautambui mipaka. 

Vilevile alihimiza wadau wengine wa sekta ya posta kuwezesha huduma za posta kuwa za kiubunifu zaidi, salama, za kuaminika, nafuu na zinazofaa wananchi. 


No comments