JUHUDI ZA NECTA KUGUNDUA CHANGAMOTO ZA KKK



Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeanika hadharani changamoto nzito zinazowakabili wanafunzi katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), hali iliyopelekea Serikali kuchukua hatua za dharura na za kimkakati. 

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, amebainisha changamoto hizo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa KKK kwa watoto wa awali na madarasa ya kwanza na pili. 

Alisema kupitia upimaji uliofanywa tangu mwaka 2015 katika halmashauri zote nchini, imebainika kuwa bado kuna vikwazo vya kitaluma vinavyozuia wanafunzi wengi kufikia umahiri unaotakiwa mapema.

Katika stadi ya kusoma, Dk. Mohamed alieleza kuwa wanafunzi wengi wanapata taabu kusoma maneno yenye herufi za ving’ong’o kama ng’ambo na ng’ombe kwa sababu ya kutumia njia ya mdomo kutoa hewa badala ya pua. 

Aidha, athari za lugha mama za kikabila zimeonekana kuwa kikwazo kikubwa katika kutofautisha matamshi ya herufi ‘R’ na ‘L’, huku wanafunzi wengi wakishindwa kufikia kasi ya kusoma maneno hamsini kwa dakika moja. Upande wa kuandika, changamoto zilibainika katika muundo wa silabi zenye konsonanti pekee na mfuatano wa konsonanti, pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya herufi kubwa na ndogo.

Kwenye stadi ya kuhesabu, Baraza limebaini changamoto zilikuwa katika kubaini namba zinazokosekana, kujumlisha namba zinazohitaji kubeba au kutoa namba zinazohitaji kukopa pamoja na kutambua maneno yanayowakilisha matendo ya kihisabati kama vile kupungua, kubaki, tofauti na ongezeko wakati wa kufumbua mafumbo. 

Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Necta ilichukua hatua ikiwamo kutoa mafunzo kuhusu upimaji wa KKK yalitolewa kwa walimu wa elimu ya awali wa darasa la kwanza na la pili, maofisa elimu taaluma, wakuu wa shule za msingi, walimu wa taaluma, maofisa elimu kata pamoja na wathibiti ubora katika mikoa na halmashauri zote nchini.

Alisema mafunzo hayo yamesaidia kuimarika kwa ufaulu katika ngazi ya upimaji wa darasa la nne na mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Hata hivyo, ili kutorudia makosa ya kuwatambua wanafunzi wenye mapungufu wakiwa tayari wamechelewa darasa la nne, NECTA iliendesha upimaji wa kwanza wa kitaifa wa darasa la pili mwezi Novemba mwaka jana katika shule 20,864 nchini, ambapo wanafunzi zaidi ya milioni 1.7 walipimwa umahiri wao. 

Aidha, Dk Mohamed alipendekeza kuwa katika mabadiliko ya kisera yanatakiwa majibu ya kisayansi kutatua changamoto za KKK ikiwamo kupambana na ugonjwa wa kuogopa namba, kuacha dhihaka kwa somo la Hisabati na kufanya mbinu za ufundishaji kuwa wa vitendo zaidi.

Kutokana na majibu hayo ya kisayansi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa KKK ili kuhakikisha watoto wanamiliki stadi hizi kabla ya kufika darasa la tatu.

Rais Samia amesisitiza kuwa KKK ndio msingi wa ujifunzaji wote na mtoto anayekosa msingi huo hupata ugumu mkubwa katika masomo ya juu. 

Katika uzinduzi huo uliopambwa na ngoma za asili kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisutu, Rais ameielekeza Wizara ya Elimu na TAMISEMI kufanya tathmini za mapema na endelevu badala ya kutegemea taarifa pekee. 

Mpango huu wa miaka mitano unalenga kuifanya mbinu ya ufundishaji kuwa ya vitendo zaidi, kuondoa dhihaka kwenye somo la Hisabati, na kujenga taifa la wasomi wenye ushindani kuelekea Dira ya 2050.


No comments