MAMA SAMIA ATIMIZA AHADI: AZINDUA MKAKATI WA KITAIFA WA KISAYANSI WA KKK
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 29 Januari 2026, amezindua rasmi Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa Elimu ya Awali na wanafunzi wa Darasa la I na II jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo ni utekelezaji wa moja ya ahadi za siku 100 zilizotolewa na Rais Dkt. Samia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ukilenga kuhakikisha watoto wote nchini wanamiliki stadi za msingi kabla ya kufika Darasa la Tatu ili kuwawezesha kujifunza kwa ufanisi katika hatua zinazofuata za elimu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyopambwa na shamrashamra za kitamaduni, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa KKK ndio msingi wa ujifunzaji wote na kubainisha kuwa mtoto anayekosa msingi huo hubaki nyuma kielimu na kupata ugumu wa kumudu masomo ya juu zaidi.
Rais ametoa pongezi kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa maandalizi thabiti, huku akieleza kuvutiwa na mbinu shirikishi za ujifunzaji zilizoonyeshwa wakati wa uzinduzi kwa kutumia zana na nyenzo bunifu zinazopatikana nchini.
Katika kuhakikisha mafanikio ya mpango huo, Rais Dkt. Samia ameielekeza Wizara ya Elimu kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na wizara za kisekta zinazohusika na maendeleo ya awali ya mtoto.
Ameagiza kufanyika kwa tathmini za mapema na endelevu za ujifunzaji ili kubaini changamoto kwa wakati kwa kuzingatia matokeo halisi ya watoto badala ya kutegemea taarifa pekee. Pia amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha walimu kwa mbinu za kisasa na nyenzo za kufundishia, sambamba na kuimarisha ukaguzi wa elimu na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji.
Mkakati huu wa KKK ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), na mchango wa Tanzania katika kutekeleza Ajenda ya Afrika 2063 pamoja na Lengo namba Nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 4) kuhusu Elimu Bora. Rais amewatambua wadau wa maendeleo na sekta binafsi kwa mchango wao katika utoaji wa elimu nchini na kuhimiza ushiriki wao zaidi katika kufanikisha mkakati huu.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa serikali imetekeleza ahadi hiyo ya Rais kabla ya kuisha kwa siku 100 za malengo ya utekelezaji na kuongeza kuwa mkakati huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano hadi mwaka 2030/2031.
Utelezaji wa mkakati huu unaenda sambamba na maboresho makubwa ya miundombinu na rasilimali watu, ambapo ujenzi wa madarasa ya elimu msingi umeongezeka kutoka 151,315 mwaka 2021 hadi 184,850 mwaka 2025, huku jumla ya walimu 6,044 wa masomo ya sayansi na hisabati wakiwa wameajiriwa kati ya walimu 7,000 waliopangwa.










Post a Comment