Dkt. Samia na Rais Mahama wakubaliana kuimarisha ushirikiano wa afya, madini na biashara



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yuko nchini Ghana kwa ziara rasmi ambapo tarehe 22 Julai, 2026, alifanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. John Dramani Mahama, katika Ikulu ya nchi hiyo, Jubilee House, jijini Accra.

Katika mazungumzo yao yaliyogusa nyanja mbalimbali za maendeleo, viongozi hao wawili wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kwa kutekeleza kwa pamoja masuala mbalimbali ya sekta ya afya ili kuboresha ustawi wa wananchi wa nchi zote mbili.

Aidha, viongozi hao walijikita katika sekta ya madini na kubadilishana uzoefu, hususan ukizingatia kuwa nchini Ghana, asilimia 60 ya uzalishaji wa madini unafanywa na wachimbaji wadogo wakati asilimia 40 ikifanywa na wachimbaji wakubwa—mfumo ambao umekuwa chachu kubwa katika kuwanufaisha wananchi wa kawaida kiuchumi.

Kuhusu biashara baina ya Tanzania na Ghana ambayo imekuwa na muamko mdogo kwa muda mrefu, Rais Dkt. Samia na Rais Mahama waligazia umuhimu wa kuipa msukumo mkubwa kupitia fursa za usafiri. Waliongeza kuwa kuanzishwa kwa safari za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika ukanda huo wa Afrika Magharibi kumeanza kuchochea fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

No comments