Angola Yaitambua Tanzania Kama Kitovu cha Ukombozi



Mjane wa Rais wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Maria Nyerere, amekabidhiwa nishani ya heshima kutoka Serikali ya Angola kwa niaba ya mume wake.

Nishani hiyo imekabidhiwa na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingo Da Silva, katika hafla  iliyofanyika nyumbani kwa Mwalimu Nyerere Msasani, Dar es Salaam jana.

Nishani hiyo ya juu kabisa ya heshima ilitunukiwa rasmi kwa Mwalimu Nyerere Novemba 6, 2025 na Serikali ya Angola, ambapo awali ilikabidhiwa kwa balozi wa Tanzania nchini Angola kwa niaba ya familia, kabla ya kukabidhiwa rasmi jana kwa Mama Maria Nyerere.

 Akizungumza balozi huyo amesema nishani hiyo imetolewa na Serikali ya Angola kutambua mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika harakati za kupigania uhuru wa taifa hilo kutoka kwa Wareno.

" Angola imetoa nishani hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo, kama ishara ya heshima na shukrani kwa viongozi wa Afrika waliotoa mchango mkubwa katika ukombozi wetu," alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema Taifa la Tanzania limepokea kwa furaha nishani hiyo, akibainisha kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika, ikiwemo Angola.

Aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika na Tanzania ilikuwa kitovu cha harakati za ukombozi, ambapo nchi kama Angola, Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia zilianzisha kambi za wapigania uhuru na kushirikiana kwa karibu na Tanzania.





Akizungumza baada ya kupokea nishani hiyo, Mama Maria Nyerere ameishukuru Serikali ya Angola kwa heshima kubwa waliyoitoa kwa niaba ya mume wake.

 Amesema kuwa nchi za Afrika zilifanya kazi kwa mshikamano mkubwa katika kupigania uhuru wao na kwamba kila taifa linapaswa kukumbuka mwanzo wa ushirikiano huo.

Aidha aliwahimiza wananchi kutokata tamaa, akisema kuwa kazi ya kuijenga jamii ni ngumu lakini muhimu, huku akisisitiza mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja.

Naye Makongoro Nyerere, akizungumza kwa niaba ya familia, alisema Mwalimu Nyerere aliamini kuwa uhuru wa Tanzania usingekuwa kamili kama nchi nyingine za Afrika zingebaki chini ya ukoloni. 

Alisema viongozi wa harakati za ukombozi walikuwa wakikutana nyumbani kwao na Mama Maria alikuwa mstari wa mbele kuwapokea wageni hao.

Aliishukuru Angola pamoja na mataifa mengine ya Afrika kwa kutambua mchango wa Mwalimu Nyerere, akisema heshima hiyo inaonesha thamani ya mshikamano wa kweli wa Afrika.


No comments