AMANI: MTAJI NA MUHIMILI MKUU WA UCHUMI WA WAMACHINGA NA WAFANYABIASHARA NCHINI
Katika harakati za kila siku za kutafuta maendeleo ya kiuchumi, amani imetajwa kuwa ndiyo mtaji namba moja unaowawezesha wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali nchini kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Wadau mbalimbali wa sekta ya biashara, wakiwemo viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA), wamebainisha kuwa bila utulivu, jitihada zote za kujikwamua kiuchumi zinaweza kukwama na kusababisha athari kubwa kwa maisha ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa SHIUMA Mkoa wa Pwani, Filemon Maliga, anasisitiza kuwa amani ni kipaumbele cha kwanza hata kabla ya mahitaji mengine ya kibiashara. Kwa mujibu wa Maliga, utulivu wa nchi ndio unaovutia wawekezaji na kuwatia shime wateja kutoka nje na ndani ya maeneo yao kujitokeza kununua bidhaa. Anasema kuwa mshikamano uliopo hivi sasa ndio chimbuko la maendeleo ya mjasiriamali mmoja mmoja na taifa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuulinda kwa nguvu zote.
Hoja hiyo inaungwa mkono na wafanyabiashara wa masoko madogo, akiwemo Joyce Mramba kutoka Soko la Michonjo Uyaoni, Kibaha. Joyce anabainisha kuwa biashara yao inategemea uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila hofu. Anasema kuwa amani ikitoweka, wafanyabiashara ndio wa kwanza kuumia kwani hushindwa kufanya shughuli zao za kila siku, jambo linaloweza kusababisha umaskini na kurudisha nyuma ustawi wa jamii. Kwake yeye, kuombea nchi utulivu na kudumisha mshikamano ni sehemu ya kazi yake ya kila siku.
Hali kadhalika, Iddi Bundala ambaye ni Mwenyekiti wa Soko la Michonjo Uyaoni, anatoa angalizo la kipekee kuhusu uhusiano kati ya amani na mikopo. Anasema kuwa wajasiriamali wengi wanatumia mitaji ya kukopa, na hivyo amani ikivunjika, itakuwa muhali kufanya biashara na kushindwa kurejesha mikopo hiyo, jambo linaloweza kuwafikisha kwenye hatua mbaya za kisheria na kiuchumi.
Bundala ametoa wito kwa vijana kuachana na makundi yanayoweza kuhatarisha usalama wa nchi na badala yake waelekeze nguvu zao katika kujenga nchi kupitia mshikamano na amani.
Kwa mtazamo wa wadau hawa, ni wazi kuwa amani si suala la kisiasa pekee, bali ni hitaji la msingi la kiuchumi. Inapokuwepo amani, biashara zinastawi, mikopo inalipika, na wateja wanakuwa na amani ya kutumia fedha zao. Hivyo, wito wa wamachinga hawa kwa watanzania wote ni kuendeleza utulivu uliopo kama nyenzo muhimu ya kuelekea kwenye uchumi wa kati na maisha bora kwa kila mwananchi.

Post a Comment