VIONGOZI WA JAMII KIBAHA WALAANI USHAWISHI WA VURUGU, WAHIMIZA MSHIKAMANO




Viongozi wa kijamii na wadau wa sekta ya biashara katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha wametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuombea na kulinda amani ya nchi, wakisisitiza kuwa bila utulivu hakuna shughuli yoyote ya kimaendeleo inayoweza kufanyika. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao wamebainisha kuwa amani ndiyo chimbuko la uhuru wa mwananchi mmoja mmoja na chachu ya mshikamano wa kitaifa unaopelekea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) tawi la Kibaha Mjini, Jabir Makasala, amewasihi wananchi kutoichezea amani iliyopo kwani ndiyo inayomfanya kila mmoja kuwa huru kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Amesema kuwa utulivu wa nchi unajenga mazingira rafiki kwa watu wa makundi yote, wakiwemo wenye ulemavu, kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao na kuchangia katika pato la taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Soko la Loliondo Kibaha, Alex Msimbe, ameitaja amani kama mtaji namba moja kwa wafanyabiashara. Amesema kuwa sekta ya biashara inategemea mazingira tulivu ili kunawiri, na kwamba wajasiriamali hawako tayari kuona mtu au kikundi chochote kikivuruga utulivu uliopo. Amesisitiza kuwa mshikamano wa kudumu ndani ya taifa ni silaha muhimu inayowawezesha wananchi kusonga mbele kimaisha bila hofu.

Naye Katibu wa kitengo cha matunda katika soko hilo, Amina Mwinyimvua, amewataka wananchi kuachana na ushawishi wowote unaoweza kupelekea vurugu ambazo si sehemu ya utamaduni wa Watanzania. Amesema kuwa amani haina mbadala na ni jukumu la kila mmoja kuilinda kwa nguvu zote kama walivyofundishwa na viongozi wa kitaifa. Amesema kuwa kulinda amani ni kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi hazisimami na taifa linaendelea kubaki katika mstari wa maendeleo.

No comments