TAIFA STARS YAICHOMOLEA TUNISIA NA KUWEKA MATUMAINI HAI MOROCCO 2025

 



Katika dimba la Olympic kule Rabat, Taifa Stars wamepambana kiume na kulazimisha sare ya 1–1 dhidi ya miamba ya Kaskazini, Tunisia. Matokeo haya yamechanganya hesabu za kundi na kuiacha Stars ikiwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele kama mshindi wa tatu bora (best loser).

Mambo yalikuwa magumu kwa Stars kwa dakika ya 54, lakini fundi wa mpira, Feisal Salum 'Fei Toto' alifanikiwa kuchafua hali ya hewa wakati alipopiga shuti la kuhesabu  shuti zuri la kuesabu (curler) kutokea pembeni mwa kisanduku, mdundo wa mpira ukamchanganya kipa Aymen Dahmen na kutinga wavuni. Bao hilo la kusawazisha liliamsha morali ya Stars na kuwafanya Tunisia waanze kupoteza ramani.



Kabla ya hapo, Tunisia walimiliki mpira kwa asilimia kubwa lakini walishindwa kupenya ngome ya Stars. Hata hivyo, katika dakika ya 42, mambo yaliingia doa baada ya Bakari Mwamnyeto kumfanyia madhambi Hazem Mastouri ndani ya kisanduku. Baada ya mwamuzi kutazama VAR kwa muda mrefu, aliamuru ipigwe penalti. Ismael Gharbi akapiga shuti lililomshinda kipa na kuwafanya Tunisia waende mapumzikoni wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Tunisia wakaingia na mbinu ya 'kupaki basi' ili kulinda ushindi wao. Mbinu hiyo ikawagharimu kwani iliwaruhusu Stars kuanza kulisogelea lango lao mara kwa mara hadi Fei Toto alipofanya yake.

Dakika za lala salama kasi ya mchezo ilishuka. Stars wakijua kuwa alama moja ni dhahabu, walicheza kwa akili na kupoteza muda (tactical time wasting) ili kulinda sare hiyo.

Sare hii inamaanisha Tunisia wamekata tiketi ya hatua ya 16 bora wakishika nafasi ya pili, huku Tanzania ikisalia na matumaini makubwa ya kufuzu kama mmoja wa washindi wa tatu bora wanne wenye pointi nyingi.



Uganda 1-3 Nigeria



Nigeria imethibitisha nafasi yake kileleni mwa Kundi C kwa ushindi mnono wa 3-1 dhidi ya Uganda katika mchezo wao wa mwisho wa makundi uliopigwa Jumanne kwenye uwanja wa Complexe Sportif de Fès mjini Fès, na kuhitimisha rasmi safari ya Uganda katika mashindano hayo.

Super Eagles waliingia uwanjani wakiwa na ushindi mara mbili dhidi ya Tanzania na Tunisia, wakati Uganda walikuwa na nafasi ya wazi lakini walihitaji alama zote tatu.

Nigeria,  ndio walioanza kupata bao katika dakika ya 28 kupitia kwa Paul Onuachu aliyemalizia mpira akiwa karibu na lango, akielekeza mpira upande wa chini kushoto baada ya pasi safi kutoka kwa Fisayo Dele-Bashiru. Bao hilo lilikuja baada ya shinikizo la mfululizo kutoka kwa Nigeria na muda mfupi baada ya kipa wa Uganda, Denis Onyango, kufanya kazi nzuri ya kuokoa shuti la mshambuliaji huyo huyo.

Uganda walifanya mabadiliko kadhaa mwanzoni mwa kipindi cha pili, lakini kazi yao ikawa ngumu zaidi katika dakika ya 56 baada ya Salim Magoola kuoneshwa kadi nyekundu kwa kushika mpira. Nigeria walitumia vyema faida ya idadi ya wachezaji muda mfupi baadaye.

Katika dakika ya 62, Raphael Onyedika aliongeza bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia ndani ya kisanduku, akisaidiwa na Samuel Chukwueze. 

Dakika tano tu baadaye, Onyedika alifunga tena, safari hii akimalizia kutokea katikati ya eneo la hatari na kufanya matokeo kuwa 3-0, akisaidiwa tena na Chukwueze.

Licha ya kubakiwa na wachezaji kumi, Uganda waliendelea kushambulia na kupata bao la kujifariji katika dakika ya 75 kupitia kwa Rogers Mato, aliyefunga kutokea katikati ya kisanduku baada ya kupata pasi kutoka kwa Allan Okello.


No comments