DAVIDO, FRENCH MONTANA NA REDONE WANOGESHA SHEREHE ZA UFUNGUZI AFCON 2025



Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (TotalEnergies CAF AFCON 2025) yameanza rasmi Jumapili nchini Morocco, huku wasanii watatu maarufu duniani wakiteka jukwaa katika sherehe za ufunguzi zilizopambwa na maonesho ya kipekee yaliyokusudiwa kuteka hisia za watazamaji kote ulimwenguni.

Dakika chache kabla ya wenyeji Morocco kuvaana na Comoro katika mchezo wa ufunguzi kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat, wasanii French Montana, Davido na RedOne waliongoza onyesho kuu lililopewa jina la "Le Show". Onyesho hilo limebaki kuwa moja ya matukio yenye mvuto mkubwa wa picha katika historia ya AFCON, likichanganya muziki, mwanga, miondoko na alama maalum katika mpangilio uliolenga hadhira ya kimataifa inayovuka mipaka ya bara la Afrika.

Wasanii Watatu, Dunia Tatu Tofauti French Montana, aliyezaliwa Morocco na kukulia nchini Marekani, alileta ushawishi wa miondoko ya Hip-hop duniani na utambulisho wa Waafrika waishio ughaibuni. Akiwa mmoja wa wasanii wenye majina makubwa duniani waliozaliwa Afrika, uwepo wake uliashiria nafasi ya Morocco kama mwenyeji na daraja la kitamaduni kati ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Davido naye alitua kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi wa muziki barani Afrika katika kizazi cha sasa. Staa huyo wa Afrobeats kutoka Nigeria amesaidia kufikisha muziki wa Afrika kwenye majukwaa makubwa duniani, akileta sauti inayohusishwa na sherehe, kujiamini na fahari ya bara hili—sifa ambazo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linaamini zinaakisi roho ya AFCON.



Akikamilisha utatu huo alikuwa RedOne, mtayarishaji wa muziki mzaliwa wa Morocco ambaye kazi zake zimeleta mapinduzi katika muziki wa Pop duniani kote. Ushiriki wake ulisisitiza uwezo wa ubunifu wa Afrika nyuma ya pazia, ukiunganisha utambulisho wa Kiafrika na wasikilizaji wa kimataifa kupitia sauti na utayarishaji mahiri.

Onyesho kwa Ajili ya Dunia "Le Show" ilionekana kama simulizi ya picha yenye nguvu, wasanii hao watatu walipokutana katikati ya jukwaa huku wakizungukwa na mianga, ngoma, na maonesho ya kidijitali. Onyesho hilo liliandaliwa kuakisi umoja, utofauti na miondoko—maudhui ambayo ni msingi wa ujumbe wa AFCON 2025. Sherehe hiyo ya ufunguzi ilitumika kama tamko la kitamaduni na kimichezo, ikionyesha ubunifu na kujiamini kwa Afrika kwa mamilioni ya watu wanaotazama duniani kote.





Sherehe hiyo inaashiria kuanza kwa mashindano ya mwezi mzima yatakayofikia tamati Januari 18, yakihusisha timu za taifa 24 zinazochuana katika miji sita wenyeji: Rabat, Casablanca, Tangier, Marrakech, Fez na Agadir. Huku viwanja tisa vikitumika na Morocco ikiandaa fainali hizi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1988, AFCON 2025 inatajwa kuwa moja ya matoleo makubwa zaidi, ikichanganya soka la kiwango cha juu na usimulizi wa kitamaduni katika ngazi ya bara.

Wakati mpira wa kwanza ukipigwa, sherehe kubwa zaidi ya soka barani Afrika inaanza si tu kwa mabao na ushindani, bali kwa muziki, utambulisho na ujumbe uliokusudiwa kuvuma mbali zaidi ya uwanja wa kijani.

No comments