Amani ya kweli ni msingi wa maendeleo: Wataalamu wasisitiza uwajibikaji na utulivu wa kiuchumi




Mchango wa amani ya kudumu katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Tanzania umesisitizwa na wachambuzi na wananchi mbalimbali, wakitoa wito wa kuishi amani kwa matendo na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi. Kauli hizi zimetolewa kufuatia mijadala kuhusu athari mbaya za vurugu zinazojitokeza wakati wa chaguzi barani Afrika.

Dkt. Francis Daudi, mtaalamu wa masuala ya jamii, alitoa onyo kali, akisema vurugu haziwezi kutoa suluhisho la kudumu bali husababisha athari zinazodumu kwa muda mrefu, ikiwemo vifo na kuzorota kwa uchumi. Maoni haya yaliungwa mkono na Thomas Kibwana, mchambuzi wa masuala ya kijamii, ambaye alieleza athari za moja kwa moja za vurugu.

"Hatuwezi kutatua changamoto zilizopo... kwa kutumia vurugu; badala yake, tunapaswa kutatua changamoto tulizonazo kwa njia ya amani ili kuendelea mbele bila kusababisha madhara ya kiuchumi nchini."

Kibwana alitaja hasa uharibifu wa miundombinu ya usafiri, akisisitiza kuwa fedha za maendeleo zinalazimika kuelekezwa kwenye ukarabati, hali inayosababisha raia kupoteza muda wa uzalishaji.

Said Miraji, mchambuzi wa siasa, alisisitiza kuwa amani lazima ianze kwa kila mmoja, akisema haitoshi kuimba amani vinywani tu, bali tuishi amani mioyoni mwetu. Alifafanua formula ya umoja: “Umoja unajengwa kwa imani, imani inajengwa kwa usawa, na usawa unajengeka kwa kushirikiana.” Miraji alihimiza wazee kutoa mfano bora kwa vijana.

Maoni haya yanawiana na hisia za wananchi waliohojiwa.

Hollyess Mbisse   mkazi wa Dar es Salaam alisisitiza kuwa amani ni "chanzo cha maendeleo" kinachotegemea usalama na uhuru. Naye Deodatus Nyangwe  mkazi wa Dodoma  alibainisha jukumu la amani katika kukuza "uwekezaji nchini" na kuleta utulivu.

Aidha Dorcas Kipangala (Dar es Salaam) alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maisha na muhimu kwa kufikishia sauti ya wananchi kwa serikali.

Ili kudumisha amani na kuepusha vurugu zinazoharibu uchumi, Mchambuzi Miraji alitoa wito kwa serikali: "Kuhakikisha inawawajibisha viongozi wasiokuwa watendaji." Alieleza kuwa kutokuwajibika huunda changamoto za kijamii zinazoweza kusababisha mifarakano.

Kwa ujumla, wataalamu na wananchi wamekubaliana kwamba maendeleo ya taifa yanategemea uwezo wa Tanzania kudumisha amani kwa matendo na kusuluhisha changamoto zote kwa njia za amani, huku viongozi wakiwajibika kwa mahitaji ya raia.

No comments