Watuhumiwa ndugu wa mauaji ya Rapa "AKA" warejeshwa Afrika Kusini
DURBAN, Afrika Kusini
Ndugu wawili wameshtakiwa kwa mauaji ya rapa maarufu wa Afrika Kusini, Kiernan Forbes, anayejulikana kwa jina la sanaa "AKA". Ndugu hao walifikishwa kizimbani baada ya kurejeshwa nchini Afrika Kusini kutoka Eswatini.
Siyabonga Ndimande na Malusi Ndimande walirudishwa nchini humo baada ya kushindwa kwa jaribio lao la kisheria la muda mrefu la kuzuia kurejeshwa Afrika Kusini.
Forbes, msanii wa hip-hop aliyeshinda tuzo, aliuawa nje ya mgahawa katika jiji Durban mwaka 2023, pamoja na rafiki yake wa karibu, mpishi mashuhuri Tebello "Tibz" Motsoane. Ingawa Afrika Kusini ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, tukio hili la risasi lilishtua taifa.
Ndugu hao pia wameshtakiwa kwa mauaji ya Motsoane na watafikishwa kortini pamoja na washtakiwa wengine watano ambao tayari wako rumande .
Wawili hao waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Durban Jumanne wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, wakiwa wamefungwa pingu miguuni na mikononi.
Wakati wa mauaji yake, Forbes alikuwa akijiandaa kwa ajili ya shoo ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.Polisi walielezea shambulio hilo kama "njama iliyoratibiwa" (coordinated hit). Ingawa inaaminika kuwa Forbes alikuwa ndiye mlengwa pekee na Motsoane alikuwa mwathirika asiyetarajiwa, nia ya mauaji bado haijabainishwa wazi.
Baba yake rapa huyo, Tony Forbes, aliiambia vyombo vya habari vya ndani kuwa anafurahishwa na maendeleo ya kesi hiyo, lakini bado ana maswali kuhusu ni nani aliyeagiza mauaji ya mwanawe na nia yao.
Mama yake, Lynn Forbes, aliweka picha yake na mwanawe kwenye Instagram akiandika: "Hewa hii ya Afrika Kusini inaniminya leo... Siwezi kupumua."
Forbes alikuwa mmoja wa wasanii wa hip-hop waliopendwa zaidi nchini Afrika Kusini baada ya kutoa albamu tatu za solo. Pia anatambulika kwa kushirikiana na wasanii wengine, ikiwemo Burna Boy wa Nigeria.
Ndugu wa Ndimande watarejea mahakamani Novemba 25 kwa ajili ya usikilizwaji wa ombi la dhamana. Kesi dhidi ya washtakiwa wenzao itaendelea katika Mahakama Kuu ya Durban mwaka ujao.

Post a Comment