Tanzania yaporomoka viwango vya FIFA
TANZANIA imeporomoka kwa nafasi tano kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mwezi wa Novemba.
Tanzania iliyokuwa nafasi ya 107 mwezi uliopita, imeshuka hadi nafasi ya 112, baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 4-3 na Kuwait katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Novemba 15, 2025 Ismailia, Misri.
Anguko hilo kwenye ubora wa FIFA, linazigusa pia Kenya na Uganda. Uganda iliyokuwa nafasi ya 83 imeshuka mpaka nafasi ya 85, wakati Kenya ikiporomoka kutoka nafasi ya 109 hadi ya 113.
Morocco ambayo kidunia imepanda hadi nafasi ya 11 kutoka nafasi ya 12 ambayo ilikuwepo awali, bado inaendelea kuwa kinara kwa Afrika ikifuatiwa na Senegal.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imepanda nafasi nne kutoka ya 60 hadi ya 56, baada ya kufanya vizuri katika mechi za mchujo kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani Ukanda wa Afrika kwa kuzifunga Cameroon na Nigeria.
Hakuna mabadiliko katika nafasi nne za juu ambapo timu nne zilizokuwa zimebaki kama zilivyokuwa kinara ni Hispania, Argentina imeendelea kushika nafasi ya pili na nafasi ya tatu ni Ufaransa, huku ya nne ikishikwa na England.

Post a Comment