VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamezidi kuukaribia
ubingwa baada ya jana kuibuka na pointi zote tatu kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi
ya Yanga katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Bao hilo pekee lililoifanya Simba kuzidi kuukaribia ubingwa
ambao kwa mara ya mwisho waliutwaa katika msimu wa mwaka 2011-12, lilifungwa na
Erasto Nyoni katika dakika ya 37 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu
uliopigwa na Shiza Kichuya na kuparazwa na Rafael Daud na kumkuta mfungaji.
Yanga walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake
Hassan Kessy kutolewa baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kutokana na
kumchezea vibaya Asante Kwasi katika dakika ya 48.
Pamoja na kucheza pungufu, lakini Simba walishindwa kutumia
nafasi hiyo kupata bao jingine na badala yake kila dakika zilipotokomea,
waliendelea kucheza kwa kujihami zaidi na kurudi nyuma.
Hatahivyo, Simba ndio walitawala zaidi mchezo huo, ambapo
walipata jumla ya kona nane wakati watani zao Yanga hawakupata kona yoyote huku
Yanga wakiwa nakadi mbili za njano wakati Simba moja na washindi walipiga
mashuti matano yaliyolenga bao wakati Yanga mawili tu.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 62 na sasa kuhitaji
pointi sita tu ili kujihakikishia ubingwa kwani Yanga akishinda mechi zake zote
sita zilizobaki atafikisha pointi 66 tu, ambazo zitakuwa zimepitwa na Wekundu
wa Msimbazi.
Baada ya kipigo hicho, Yanga wanaendelea kuwa katika nafasi
ya tatu wakiwa na pointi zao 48 wakiwa pointi moja nyuma ya Azam FC, ambayo iko
katika nafasi ya pili licha ya kucheza mechi 26 wakati Yanga wamecheza jumla ya
mechi 24.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nyoni ambaye alifunga bao
hilo pekee alisema kuwa wao wamepania kila mechi kupata pointi tatu na
alifanikiwa kufunga bao hilo baada ya mabeki wa Yanga kuwabana wafungaji wa
Simba, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco.
Endapo Simba itatwaa ubingwa wa Tanzania Bara, itapata
nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika
msimu ujao.
Kikosi
Simba kilikuwa: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Nicholas
Gyan/ Paul
Bukaba, Yusufu Mlipili, James Kotei, Jonasi Mkude, Asante Kwasi, Shomari
Kapombe, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.
Yanga:Youthe
Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Said
Makapu, Yusuph Mhilu, Papy Tshishimbi/Emmanuel Martin, Obrey Chirwa, Raphael
Daud/ Juma Mahadhi na Ibrahim Ajibu/
Pius Buswita.
Msimamo:
MP W D L GF GA +/- Pts
Simba 26 18 8 0 59 13 46 62
Azam 26 13 10 3 25 12 13 49
Yanga 24 13 9 2 40 14 27 48
Prisons 25 9 11 5 22 18 4 38
Singida 26 9 11 6 23 24 -1 38
Mtibwa 25 8 9 8 20 19 1 33
Lipuli 26 7 11 8 19 20 -1 32
Ruvu 26 8 8 10 26 33 -7 32
Stand 26 7 8 11 19 30 -11 29
Mbeya City 26 5 13 8 23 30 -7 28
Kagera Sugar 26 5 12 9 17 25 -8 27
Mwadui 25 5 11 9 27 34 -7 26
Mbao 25 5 9 11 23 33 -10 24
Majimaji 26 4 11 11 26 36 -10 23
Ndanda 26 4 11 11 17 28 -11 23
Njombe Mji 26 4 10 12 16 33 -17 22
No comments:
Post a Comment