YANGA imepangwa
kucheza na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mechi ya mchujo ya michuano ya
Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa ratiba
iliyopangwa makao makuu ya Shirikisho la soka Afrika (CAF), Cairo Misri leo Yanga itakuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza mapema mwezi ujao kwenye uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Kufikia hatua hiyo,
Dicha iliitoa Zamalek ya Misri baada ya kila mmoja kushinda mabao 2-1 kwao
kabla ya kuwatoa mabingwa hao wa zamani wa Afrika kwa matuta.
Kabla ya kucheza na
Zamalek, ilicheza na Zimamoto ya Zanzibar na kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika
mechi ya kwanza Zanzibar kabla ya kushinda bao 1-0 nyumbani Ethiopia.
Dicha inaonekana ni
timu dhaifu kwani inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya
Ethiopia inayoshirikisha timu 16 ikiwa na pointi 19 katika mechi 15 ilizocheza.
Yanga imeangukia
kwenye michuano hiyo baada ya kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa
jumla ya mabao 2-1 iliyofungwa nyumbani uwanja wa Taifa na Township Rollers ya
Botswana kabla ya kwenda kulazimisha suluhu ugenini Gaborone.
Mwaka juzi Yanga pia
ilishiriki michuano hii baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Al Ahly
ambapo ilicheza na Esperanca ya Angola kwenye kombe la Shirikisho na kufuzu
hatua ya makundi.
No comments:
Post a Comment