NAIBU WAZIRI MAKONDA AWAPA MORALI TAIFA STARS




Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, ametoa hamasa na morali kwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) pamoja na benchi la ufundi, alipokutana nao katika hoteli ya Barcelo Convention Center, jijini Fes, Morocco, ambako timu hiyo imeweka kambi ya maandalizi.

Akizungumza na wachezaji na benchi la ufundi, Mhe. Makonda aliwasisitiza wachezaji kupambana kwa moyo wote, nidhamu na uzalendo wanapoivaa jezi ya Taifa, akibainisha kuwa Watanzania wote wako nyuma yao kwa kuwaunga mkono, kuwashangilia na kuwaombea ili waweze kuliletea Taifa heshima.

“Taifa zima lina imani kubwa nanyi. Chezeni kwa moyo, kwa umoja na kwa kujituma, mkijua mna mamilioni ya Watanzania wanaowaombea na kuwaunga mkono,” alisema Mhe. Makonda.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo, Bw. Abel Philip, Bw. Alex nkeyenge Mkurugenzi Msaidiza Idara ya Michezo pamoja na Profesa Madundo Mtambo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya AFCON 2027.

Kwa upande wa wachezaji walimshukuru Mhe. Makonda na ujumbe wake kwa kuwatembelea na kuwapa moyo, wakiahidi kupambana kwa nguvu zao zote uwanjani.

Taifa Stars inatarajiwa  kucheza mchezo wa kwanza tarehe 23 Desemba, 2025, katika mji wa Fes, Morocco, dhidi ya Timu ya Taifa ya Nigeria.

No comments