TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri
wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo imeshinda mabao 2-1 dhidi ya wenzao wa
Msumbiji katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Huo ni ushindi wa pili kwa Ngorongoro katika
mechi za kirafiki za kimataifa baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuifunga
Morocco bao 1-0.
Katika mechi hiyo, wageni Msumbiji walikuwa
wa kwanza kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 13 likiwekwa kimiani na
Martinho Alberto kwa mkwaju wa penalti baada ya kipa wa Ngorongoro Aboutnalib
Mshery kumchezea vibaya mchezaji wa Msumbiji aliyekuwa akielekea kufunga.
Mshambuliaji Abdul Suleiman aliisawazishia Ngorongoro bao
baada ya kuunganisha pasi ya Said Bakari akiwa ndani ya 18 na kwenda mapumziko
wakiwa sare ya bao 1-1.
Dakika ya 59 nusura Ngorongoro ipate bao la
mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi baada ya mchezaji wake kuchezewa
vibaya na wa Msumbiji, lakini Hasad Juma aliyepewa dhamana ya kupiga penalti
hiyo alikosa.
Bao la pili la vijana hao wa kocha Amy Ninje
lilifungwa dakika ya 69 na Said Bakari kwa shuti kali ndani ya 18.
Baada ya mechi hizo, Ngorongoro sasa
inajiandaa na mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana wa umri huo
dhidi ya Congo DR mwishoni mwa mwezi huu kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment