AFCON 2025 MOROCCO KUVUNJA REKODI: TIKETI MILIONI 1 'ZAYAYUKA'



Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limetangaza kuwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 itakayofanyika nchini Morocco, inatarajiwa kuwa mashindano bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya bara hili.

Akizungumza jijini Rabat, Katibu Mkuu wa CAF, Véron Mosengo-Omba, amesema viashiria vyote vinaonyesha kuwa toleo hili litavunja rekodi zote zilizowekwa awali, kuanzia miundombinu, mahudhurio ya mashabiki, hadi mapato.

Rekodi ya Tiketi na Viwanja

Kwa mara ya kwanza, AFCON itashuhudia matumizi ya viwanja tisa (9) vyenye hadhi ya kimataifa katika miji sita tofauti (Rabat, Casablanca, Tangier, Agadir, Fez, na Marrakech). Mosengo-Omba alibainisha kuwa hamasa ni ya kipekee ambapo zaidi ya tiketi milioni moja tayari zimeshauzwa kabla ya mashindano kuanza.

"Hatujawahi kuwa na AFCON yenye hamasa kubwa kiasi hiki. Kuuza tiketi milioni moja mapema hivi ni kiashiria tosha kuwa huu utakuwa msimu wa kipekee," alisema Katibu huyo.

Soko la Kimataifa na Vyombo vya Habari

Mvuto wa AFCON 2025 umevuka mipaka ya Afrika. CAF imethibitisha kuwa:

Nchi 30 za Ulaya zitaonyesha mashindano hayo mbashara (ongezeko la nchi 18 mpya).

Nchi zote 54 za Afrika zitatangaza michuano hiyo.

Zaidi ya wanahabari 3,800 tayari wameshathibitishwa kwenda kuripoti tukio hilo.

Maandalizi ya Morocco

CAF imemshukuru Mfalme Mohammed VI kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu, huku Uwanja wa Prince Moulay Abdellah ukitajwa kuwa "makumbusho ya kisasa" kutokana na ubora wake.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (FRMF), Mouad Hajji, amesisitiza kuwa wamejipanga vyema upande wa usafiri (barabara na reli) na hoteli ili kuhakikisha mashabiki wanapata huduma bora kabisa.


No comments