MZAMIRU Yassin na
Emmanuel Okwi leo waliinyoosha Njombe Mji baada ya kuchangia ushindi wa mabao
4-0 kwa Simba katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Uhuru Dar es
Salaam.
Katika mechi hiyo,
Yassin alifunga mabao mawili na Okwi akifunga moja huku akitengeneza mengine
mawili na Laudit Mavugo akifunga bao la nne kwa Simba.
Ni kama Okwi
anawanyoosha mashabiki wanaomkebehi kwamba amezeeka na kumuita Mhenga,
kwani mpaka sasa amefunga mabao nane huku timu yake ikiwa na mechi saba.
Simba imepata ushindi
huo ikiwa zimesalia wiki moja kabla ya mechi dhidi ya wapinzani wake Yanga
kwenye uwanja wa Uhuru mwishoni mwa wiki ijayo.
Matokeo hayo yanaifanya
Simba inayohaha kusaka ubingwa kwa takribani mwaka wa tano sasa, kujikita
kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba.
Okwi alifunga bao la
kuongoza kwa Simba katika dakika ya 27 baada ya kuunganisha mpira wa krosi ya
Erasto Nyoni kabla ya kuujaza mpira wavuni akiwa amefikisha bao la nne msimu
huu.
Simba iliyoonekana kuwa
bora zaidi kwani ilifika langoni mwa Njombe Mji mara kwa mara huku
wachezaji wake akiwemo Shija Kichuya wakikosa mabao kadhaa na kwenda mapumziko
wakiwa mbele kwa bao hilo.
Njombe walianza kipindi
cha pili wakiwa dhaifu zaidi ya kipindi cha kwanza na hapo safu ya ushambuliaji
ya Simba haikufanya kosa na ndipo Mzamiru Yassin alipoandika bao la pili katika
dakika ya 51 na dakika mbili baadae aliongeza la tatu. Mabao yote hayo
akiunganisha pasi za ‘Mhenga’ Okwi.
Dakika ya 59, Laudit
Mavugo alifunga bao la nne akiunganisha pasi ya Kichuya.
Baada ya mechi ya leo,
Simba kesho itafanya safari ya Zanzibar kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Yanga
Jumamosi.
Naye Alexander Sanga
kutoka Mwanza anaripoti kuwa Mbao imetoka suluhu na Azam kwenye uwanja wa CCM
Kirumba.
Mechi nyingine
zilizochezwa jana, Lipuli ikiwa nyumbani imeichapa Majimaji bao 1-0 Mbeya City
imeifunga Ruvu Shooting mabao 2-0 kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, Ndanda
ikitoka suluhu na Singida United na Mtibwa Sugar ikishinda bao 1-0 dhidi ya
Prisons.
Mtibwa imeendelea
kushika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa pointi sawa na Simba, ikizidiwa
mabao.
No comments:
Post a Comment