MKUU wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda ametatua changamoto zilizokuwa zinakikabili Chama cha
Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), kwa kuwapa jenereta, mipira na
mabati huku akiwataka kuhakikisha
wanafanya vizuri kitaifa na kimataifa.
Hiyo ni ahadi
aliyowahi kuwaahidi baada ya kutembelea katika mashindano ya ligi ya mkoa na
kuelezwa changamoto ya kukatika kwa umeme wakati mechi ikiendelea na mabati
kuvuja maji mvua zikinyesha na kusababisha mchezo kusimama.
Akikabidhi vifaa
hivyo jana Dar es Salaam Makonda alisema BD waliomba jenereta la KV 25 lakini
ameamua kutoa la KV 35 litakalofanya kazi muda mrefu, lakini pia, waliomba mabati 100 na kuamua kuwapa 150 na mipira 110
ili kusaidia kuendeleza mchezo huo.
Makonda alisema
anataka kuona mchezo huo na mingine yote iliyoko katika mkoa wake kama
netiboli, wavu na kuogelea inafanya vizuri ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Niliona namna
mnavyotaabika nikaona niwatie moyo kwa kuwa kuna vijana wengi wanatamani
kucheza mchezo huo wapate nafasi ya kushiriki, nategemea michezo yote Dar es
Salaam itafanya vizuri pia,” alisema.
Pia, alisema ahadi
yake ya kujenga viwanja vitatu vya mchezo huo ipo kama kawaida na muda wowote
atasaini mkataba na wakandarasi kuanza mchakato wa ujenzi.
Pia, alitangaza neema
katika mchezo wa kuogelea akiahidi kujenga bwawa moja la kisasa la kimataifa
ili pia, mchezo huo ufanye vizuri zaidi.
Aliahidi kushirikiana
na viongozi wa BD na wengine, kuhakikisha anatimiza ahadi zake huku pia,
akiahidi kuunda Kamati maalumu itakayoshughulikia michezo yote ndani ya mkoa na
kutatua changamoto zao.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa BD, Okare Emesu alimuahidi mkuu huyo kuwa watahakikisha wanafanya
vizuri na kuutangaza mkoa katika ngazi ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment