KOCHA raia wa Sweden, Mariane Sundhage amesema Tanzania ina vipaji vya soka ila vinahitaji
kuendelezwa.
Sundhage aliyasema
hayo jana wakati wa kliniki ya soka kwa wachezaji wa kike iliyofanyika katika
Uwanja wa Karume Dar es Salaam.
"Jana (juzi)
nilikuwa Morogoro nimeona wachezaji chipukizi, wana vipaji na wanapenda soka
cha msingi ni kuendelezwa na naamini wakiendelezwa baada ya miaka kadhaa
mtakuwa na wachezaji wanaocheza soka nje ya Tanzania," alisema Sundhage.
Aliwaasa wachezaji
kufanya mazoezi kwa bidii ili kukuza kipaji, kula vizuri na kupata muda wa
kutosha kupumzika.
Awali akizungumza
kwenye kliniki hiyo, Mwenyekiti wa Chama
cha soka la wanawake (TWFA), Amina Karuma alisema Kamati ya soka la wanawake
inapambana kuona mpira wa miguu unachezwa kila kona ya Tanzania ndio maana
imemleta Sundhage na hivi karibuni ligi ya wanawake itachezwa katika msimu wa
pili.
"Kamati kwa
kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini tunajitahidi kuhakikisha
soka la wanawake linachezwa ndio maana tumemleta kocha Sundhage," alisema
Karuma.
Pia Karuma aliwataka
wachezaji waliopo Twiga Stars kuendelea na mazoezi kwani hivi karibuni
wataingia kambini kujiandaa na mashindano ya Cecafa.
No comments:
Post a Comment