TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetwaa
medali ya shaba baada ya kuifunga kwa penalti Lesotho katika mchezo wa kusaka
mshindi wa tatu katika Kombe la Cosafa.
Mchezo huo ilibidi bingwa apatikane kwa penalti
baada ya timu hizo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na zile 30 za
nyongeza.
Kwa ushindi huo, Taifa Stars imepata dola za
Kimarekani 10,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 22) na kutwaa medali ya shaba katika
mashindano hayo.
Tanzania katika mchezo huo iliibuka na ushindi wa
mabao 4-2 dhidi ya Lesotho baada ya kupigiana penalti baada ya kumalizika kwa
mchezo huo.
Katika mchezo mwingine wa kusaka nafasi ya nne na
tano, wenyeji Afrika Kusini walipata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya
Namibia katika mchezo uliochezwa mapema juzi.
Lesotho ilikosa nafasi kibao licha ya kutawala
mchezo huo baada ya kushindwa kuutumbukiza mpira ndani ya kimia.
Huo ulikuwa ni mchezo wa tatu wa Lesotho katika
mashindano hayo, ambayo ilianzia hatua ya robo fainali, wakati Tanzania huo
ulikuwa ni mchezo wake wa sita ndani ya wiki mbili.
Katika kipindi cha kwanza kiungo anayecheza soka
Marekani, Thabantso Jane shuti lake lilipoteza mwelekeo huku Kefuoe Mahula na
Sera Motebang nao wakipoteza nafasi za wazi.
Taifa Stars nao nusura wapate bao katika dakika za
mwisho za mchezo lakini Mzamiru Yasin alipaisha juu ya lango.
Shujaa wa Taifa Stars alikuwa kipa Said Mduda
aliyepangua penalti ya nahodha wa Mamba hao, Thapelo Mokhehle baada ya Sera
Motebang kugongesha kwenye mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na
Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya
kwanza ya Tanzania.
Walioifungia Taifa Stars ni nahodha Himid
Mao,Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi na kupata ushindi wa 4-2.
Ushindi wa Stars kwa Lesotho umekuja siku 25 baada
ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L
kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es
Salaam.
Fainali ya Cosafa Castle 2017 itachezwa leo kwenye
Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg kati ya Zambia na Zimbabwe
na bingwa atapata dola 42,000 na mshindi wa pili dola 21,000.
Katika safari yake ya Kombe la Cosafa, Taifa Stars
iliifunga Malawi 2-0, ikatoka suluhu na Angola, huku ikitoka sare ya 1-1 na
Mauritius kabla ya kuifunga Afrika Kusini 1-0 na kufungwa na Zambia kwa penalti
4-2.
No comments:
Post a Comment