FAINALI za 31 za
mashindano ya Mataifa ya Afrika, yaani Afcon zinaanza leo nchini Gabon na
kushirikisha nchi 16 ikiwemo mwenyeji Gabon iliyofuzu kutokana na uenyeji wake.
Ukiondoa mwenyeji
Gabon, timu zingine zote 15 ikiwemo Ivory Coast ambaye ni bingwa mtetezi,
zilianzia katika hatua ya kufuzu ili kusaka nafasi ya kushiriki katika fainali
hizo.
Ni fainali za 31
na Tanzania ilishiriki mara moja tu mwaka 1980 nchini Nigeria, ambapo
mashindano hayo yalishirikisha timu nane, ambazo ziligawanywa katika makundi
mawili ya timu nne kila moja.
Kwa sasa kuna
jumla ya timu 16, ambazo zinagawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila
moja.
Fainali hizo
zinafanyika huku Tanzania ikiendelea kutokuwepo katika fainali hizo kwa mara
nyingine tena baada ya kushindwa kufuzu baada ya timu ya Taifa Stars kuchemka.
Kuanzia leo
tutashuhudia mipambano ya aina yake kutoka kwa nyota wa soka wanaocheza soka
Ulaya, China, Marekani na Afrika ambao wamejaa vipaji.
Wachezaji wa timu
za Tanzania ziwe za klabu au za taifa wana kitu cha kujifunza kutoka katika
mashindano hayo makubwa kabisa ya taifa barani Afrika.
Mashindano hayo
yana wachezaji nyota kama vile akina Riyad Mahrez, Islam Sliman na Daniel Amertey,
ambao wanacheza soka katika klabu ya England ya Leicester City ya England.
Hao ni wachache
kwani kuna wachezaji wengi zaidi nyota ambao watashiriki katika mashindano hayo
ya Mataifa ya Afrika.
Kikubwa wachezaji
wa Tanzania wanatakiwa kujifunza kitu kutoka kwa wachezaji na timu za taifa
zinazoshiriki mashindano hayo ya Afcon.
Lakini cha ajabu
utashangaa kuona wachezaji wa Tanzania badala ya kujifunza mbinu za uchezaji
kutoka kwa wenzao wa Afcon, badala yake wataiga unyowaji wa nywele na ulegezaji
bukta utakaofanywa na baadhi ya wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo.
Katika Afcon
kutakuwa na mbinu kibao za uchezaji soka, ambazo ndizo zinatakiwa kuigwa na
wachezaji wetu ili watuoneshe ufundi katika Ligi Kuu Tanzania Bara na wale
waliopo katika Taifa Stars.
Watanzania
hawataki kuoneshwa mitindo ya ulegezaji bukta au kunyoa viduku, kuweka tatuu na
badala yake wanataka kuona mitindo ya soka la kisasa.
Wachezaji wa
Tanzania tuache kuiaga ujinga na badala yake muige vitu vya msingi, ambavyo
vitawasaidia kuboresha au kunoa viwango vyenu vya mchezo na sio kulegeza bukta.
Wachezaji wetu ni
mahiri sana kuiga vitu vya kijinga, ambavyo wanavipatia kweli, lakini
linapokuja suala la kiwango cha mchezo wanashindwa kuiga wenzao wanavyofanya
vizuri.
Baada ya kukosa
mwakilishi katika Afcon, lakini sasa Watanzania watafarijika kwa msanii wao
Diamond kutumbuiza katika ufunguzi wa Afcon 2017.
No comments:
Post a Comment