LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 34 (Pamba vs Friends
Rangers). Kamishna wa mechi hiyo Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti
kitendo cha timu ya Pamba kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match
meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume
na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 35 (Kiluvya United vs
Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi
ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne.
Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw.
Athuman Mzongela anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka
kuwapiga wakati wa mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha
chafu waamuzi na Msimamizi wa Kituo.
Mechi namba 36 (African Sports vs
Ashanti United). Daktari wa Ashanti United, Andrea Mbuguni amefungiwa miezi
sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya
kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba moja.
Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano
FC). Kocha wa Mshikamano FC, Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa
faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa
nyongeza wa dakika tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu
hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji wa Mshikamano FC, John
Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven
Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson
A. Msuya.
Lakini pia Mwamuzi Bryson A. Msuya
amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti
dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.
Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo
Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga
vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa
akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti
dhidi yao.
Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni
ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Mwamuzi Katuma pia alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea
kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza.
Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba
ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti
na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya
38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kamishna wa mechi hiyo Fidelis
Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya makamishna kwa taarifa yake
kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya
39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Makamishna.
Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo
vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia
viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.
Uwanja wa Kichangani umeondolewa
kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia
Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo
ulikuwa kwenye matengenezo ambayo tayari yamekamilika.
Mechi namba 39 (Polisi Dar vs Pamba
FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa kutofika kwenye kikao cha maandalizi
ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya
Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 33 (KMC vs JKT Mlale).
Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa
lugha chafu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la
Kwanza.
Mechi namba 38 (Kimondo FC vs Njombe
Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini
ya sh. 300,000 kwa kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji
wake wajiangushe ili kupoteza muda.
Mechi namba 40 (Coastal Union vs
Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi; Kipa Hamza Mpatula na Optatus
Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa
kosa la kupigana wakiwa uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni
uzingativu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa
Wachezaji.
Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs
Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa
kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya
14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs
Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo, Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu
zikielekea vyumbani baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina
Faso). Klabu ya Burkina Faso imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria
kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya
14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 18 (Cosmopolitan vs
Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC imepigwa faini ya sh. 200,000
kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya
filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja
la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 19 (Kariakoo vs
Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na
daktari katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).
Mechi namba 16 (Sabasaba vs
Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali kutokana na washabiki wake
kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani baada ya mechi hiyo iliyochezwa
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya
42(1) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 17 (Mawezi Market vs
Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria
kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na pia kuchelewa kufika
uwanjani kwa dakika 35. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja
la Pili.
Mechi namba 19 (Namungo vs Mighty
Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji
wa akiba na viongozi wake kuingia uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo
hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya
14(47) ya Ligi Daraja la Pili.
No comments:
Post a Comment