JUHUDI za
Yanga kupata ushindi wa kwanza na kufufua matumaini ya kutinga nusu fainali ya
michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) hazijazaa matunda,
baada ya jana kutoka sare ya bao 1-1 na Medeama ya Ghana, Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Kutokana na
matokeo ya mchezo huo, Yanga inaendelea kushika mkia ikiwa na pointi moja
katika kundi lake baada ya kumaliza duru la kwanza la michuano hiyo kwa kucheza
michezo mitatu, wakati Medeama imefikisha pointi mbili na inashika nafasi ya
pili kutoka mkiani.
Yanga
ilianza michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na Mouloudia Olympique Bejaia (MO
Bejaia) nchini Algeria kabla ya kufungwa 1-0 na TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) mjini Dar es Salaam.
TP Mazembe
inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita baada ya kushinda michezo yake miwili
iliyopita dhidi ya Medeama na Yanga, wakati MO Bejaia inashika nafasi ya pili
ikiwa na pointi nne.
MO Bejaia
iliifunga Yanga bao 1-0 na kutoka sare na Medeama, ambapo leo itaikaribisha TP
Mazembe katika kukamilisha duru la pili la michuano hiyo.
Yanga bado
ina nafasi ya kufanya vizuri katika
michuano hiyo, lakini itabidi ihakikishe haipotezi mechi zake tatu zilizobaki
za duru la pili.
Duru la pili
linatarajiwa kuanza Julai 26, ambapo Yanga itakuwa ugenini nchini Ghana
kurudiana na Medeana, wakati TP Mazembe itaikaribisha MO Bejaia.
Kihesabu,
Yanga itabidi iombe TP Mazembe ishinde leo, kisha yenyewe mchezo ujao nayo
ishinde ifikishe pointi nne sawa na MO Bejaia, huku pia ikiomba Mazembe iifunge
tena MO Bejaia zitakaporudiana.
Kama matokeo
yakiwa hivyo ina maana tayari TP Mazembe itakuwa imekamata nafasi ya kwanza,
ambapo Yanga, MO Bejaia na Medeama zitakuwa zinawania nafasi ya pili.
Katika
mchezo wa jana, Yanga ilipata bao dakika ya kwanza tu mfungaji akiwa Donald
Ngoma baada ya Simon Msuva kuingia katika eneo la hatari na kutoa pasi kwa
mfungaji.
Kuingia kwa
bao hilo kuliwapa imani mashabiki wa Yanga kwamba huenda timu yao ingeibuka na
ushindi mnono zaidi hasa kutokana na Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm kuwahi
kuinoa Medeama hivyo kuifahamu vizuri, lakini wageni walitulia na kufanya
mashambulizi ya kushtukiza.
Medeama
ilisawazisha dakika ya 17, mfungaji akiwa Benard Danso akiunganisha mpira wa
kona huku beki Vicent Bossou na kipa Deogratius Munishi wakibaki wameduwaa.
Kwa ujumla
kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu huku wageni wakifanya
mashambulizi ya kushtukiza zaidi, wakati Yanga ikipoteza nafasi nyingi za
kufunga.
Yanga
itabidi ijilaumu kutokana na kushindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata kipindi
cha pili ama kwa kushindwa kulenga lango au kupiga mipira iliyookolewa na kipa
wa Medeama.
Moja ya
nafasi hizo ni ile ya dakika ya 70, ambapo shuti la kiungo Thabani Kamusoko
liliokolewa na kipa, ambapo dakika tatu baadaye Ngoma alishindwa kufunga kwa
kichwa.
Nafasi
nyingine nzuri kwa Yanga ilikuwa dakika ya 59 wakati Juma Abdul alipoingia
katika eneo la Waghana na kupiga krosi kwa Ngoma, lakini tiktak aliyopiga
mshambuliaji huyo iliokolewa na kipa wa Medeama.
Yanga: Deogratius
Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Juma Mahadhi, Kelvin Yondani, Vincent
Bossou, Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Obrey Chirwa, Amissi
Tambwe/Haruna Niyonzima na Ngoma.
No comments:
Post a Comment