TAIFA STARS YALALA 2-1 KWA NIGERIA
.Senegal na DR Congo Zaanza kwa Kishindo
Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, imeanza kampeni yake vibaya baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Nigeria ‘Super Eagles’ katika mchezo wa kundi lao uliopigwa Complexe Sportif de Fès chini ya refarii Dahane Beida..
Nigeria walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 36 kupitia kwa mlinzi Semi Ajayi, aliyepiga kichwa kikali kufuatia krosi ya Alex Iwobi. Stars walirudi kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha katika dakika ya 50 kupitia kwa Charles M’Mbowa, aliyemalizia pasi safi kutoka kwa Novatus Dismas.
Hata hivyo, furaha ya Watanzania ilidumu kwa dakika moja pekee, kwani mchezaji bora wa Afrika wa mwaka 2024, Ademola Lookman, alifunga bao la ushindi kwa shuti kali la ufundi lililomshinda mlinda mlango Stanley Nwabali. Licha ya juhudi za Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kutaka kusawazisha mwishoni mwa mchezo, shuti lake lilitoka nje na kuacha pointi tatu mikononi mwa Nigeria.
Semi Ajayi (Mchezaji Bora wa Mechi): "Ni hisia ya ajabu kufunga kwa ajili ya nchi yako. Tunatumia kiwango chetu cha AFCON iliyopita kama kipimo chetu. Kuna mambo ya kurekebisha lakini tunafurahi kwa ushindi huu."
Senegal 3-0 Botswana: Simba wa Teranga Wanguruma
Mabingwa wa zamani, Senegal, wameanza kwa kishindo baada ya kuishindilia Botswana mabao 3-0 mjini Tangier. Mshambuliaji Nicolas Jackson aling’ara kwa kufunga mabao mawili (dakika ya 40 na 58), huku Cherif Ndiaye akipigilia msumari wa mwisho dakika ya 90.
Senegal walitawala mchezo huo mwanzo hadi mwisho, huku kipa wa Botswana, Goitseone Phoko, akifanya kazi ya ziada kuokoa michomo ya Sadio Mane na Ilman Ndiaye ili kuzuia kipigo kikubwa zaidi.
DR Congo 1-0 Benin: Leopards Wapata Ushindi Mwembamba
Katika dimba la Al Madina kule Rabat, bao la mapema la Théo Bongonda katika dakika ya 16 lilitosha kuwapa DR Congo ushindi wa 1-0 dhidi ya Benin.
Licha ya Benin kupambana kutaka kusawazisha, safu ya ulinzi ya Wakongomani ilisimama imara. Kocha wa Benin, Gernot Rohr, alieleza kujivunia vijana wake licha ya kupoteza, akisema timu yake haikustahili kufungwa kulingana na kiwango walichoonyesha.
Matokeo kwa Ufupi:
DR Congo 1-0 Benin (Bongonda 16’)
Senegal 3-0 Botswana (Jackson 40’, 58’, C. Ndiaye 90’)
Nigeria 2-1 Tanzania (Ajayi 36’, Lookman 51’ / M’Mbowa 50’)

Post a Comment