CHELSEA ni moja ya klabu zilizopata kusajili wachezaji wengi wazuri; na
hata sasa bado wanasajili vijana wadogo na kuwatoa mkopo kwa klabu mbalimbali
maeneo tofauti duniani.
Wakati moja ya njia za klabu kujenga kikosi imara ni kuwa na msingi
katika kusajili chipukizi au kupandisha wale walio kwenye akademia zake, kuna
njia mbadala.
Njia hiyo ni kuvunja benki na kusajili wachezaji wenye majina makubwa.
Tulipata kuona wachezaji wakubwa ambao Chelsea walisajili kwa kiasi kikubwa cha
fedha na kuwafaa.
Leo hii tugeukie upande wa pili kwa kuangalia majina makubwa
waliyosajili lakini dimbani mwao wakageuka kuwa magarasa na hasara tupu kwa
klabu.
Fernando Torres
Mchezaji huyu wa Hispania aliletwa Stamford Bridge kutoka Liverpool kwa
ada iliyoshitua wengi ya pauni milioni 50.
Kocha mmoja baada ya mwingine waliotua hapo walishindwa kumtumia Torres
aliyekuwa akishuka kiwango kadiri muda ulivyokwenda, akawa tofauti kabisa na
nyota aliyekuwa Anfield.
Huyu amewekwa kwenye kundi la ununuzi mbaya zaidi katika historia ya
soka ya England. Msimu uliopita Jose Mourinho alifikwa na maji shingoni kiasi
cha kumbeza mshambuliaji huyo kwa kutoifanya kazi yake, ndipo akamuuza Atletico
Madrid alikoanzia kung’ara.
Andriy Shevchenko
Huyu ndiye aliyekuwa akiitwa ‘The Original Torres’. Shujaa huyu wa
Ukraine alipendwa sana na mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, lakini ukweli
ni kwamba kununuliwa kwake kwa pauni milioni 30 kutoka AC Milan 2006, alikuwa
si yule wa awali.
Baada ya kuingia Chelsea miguu yake ilipatwa kigugumizi mara kwa mara na
mashabiki wakashindwa kuelewa kulikoni. Ilibidi awekwe kwenye meli na
kurejeshwa Milan kwa mkopo baada ya misimu miwili tu kisha akatupiwa virago
moja kwa moja kwenda Dynamo Kiev 2009.
Chris Sutton
Huyu ni uthibitisho kwamba Chelsea walikuwa wakitumia fedha nyingi kwa
wachezaji wasiotoa matunda tarajiwa, muda mrefu kabla hata mashabiki wa soka
kumsikia Abramovich.
Chris Sutton aliwasili Stamford Bridge akitoka Blackburn kwa ada ya
pauni milioni 10 ambayo kwa mwaka 1999 ilikuwa kubwa sana. Hakupata kufufuka
tangu alipoanza kucheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Sunderland, aliposhindwa
kufunga bao la wazi kabisa akiwa na kipa Thomas Sorensen. Aliishia kufunga
mabao matatu tu katika mechi 39 ndiyo maana baada ya msimu mmoja tu alipigwa
bei kwenda Celtic.
Shaun Wright-Phillips
Kocha Mourinho angeweza kutumia vyema zaidi fedha kiasi cha pauni
milioni 21 alipoamua kwenda Manchester City kumsajili winga Shaun
Wright-Phillips.
Kuna hoja kwamba hakuwahi kupata fursa ya kweli kwa timu hiyo
japokuwa ufungaji wa mabao 10 katika mechi 124 unaweka wazi hali yake. Ni
mchezaji aliyekuwa na kipaji cha aina yake ambaye hata hivyo hakutokea kuwa
sehemu muhimu ya kikosi cha ushindi.
Juan Sebastian Veron
Raia huyu wa Argentina aliyekuwa na kipaji kikubwa aliendana na matumizi
ya kutisha yaliyokuja zama za Abramovich. Ajabu ni kwamba Chelsea waliamua
kumwaga pauni milioni 15 kwa mchezaji ambaye tayari alishaonekana garasa akiwa
na Manchester United kiwango chake kiliposhuka.
Alicheza mechi 15 tu na Chelsea kabla ya kuanza msururu wa
kutolewa kwa mkopo na kuingia kwenye vitabu vya historia kama moja ya majina
makubwa zaidi yaliyoanguka.
Winston Bogarde
Mdachi huyu aliingia akiwa mchezaji huru lakini akaishia kuwa moja ya
wachezaji hovyo zaidi kupata kusajiliwa katika historia ya Ligi Kuu.
Bogarde alishindwa kutamba klabuni hapo kwa sababu mpira ulimkataa au
aliukataa mpira licha ya kwamba alikuwa akilipwa kiasi kikubwa cha mshahara kwa
wiki – wakati ule mwaka 2000 ikiwa ni pauni 40,000 kwa wiki.
Chelsea walijaribu kumwondosha lakini akakataa kufuta mkataba wake hadi
umalizike na alikuwa akienda mazoezini akitoka Amsterdam, maana hata mechi
hakuwa akipangwa tena, alikuwa akila mshahara tu.
Adrian Mutu
Unamkumbuka Adrian Mutu? Huyu alihusika kwenye moja ya pilika za ajabu
zaidi za usajili katika historia ya Chelsea. Alisajiliwa kwa pauni milioni 15.8
lakini akafunga mabao sita tu ligi kuu.
Walau Chelsea walipata sababu ya kuachana naye, pale alipokutwa ametumia
dawa za kulevya aina ya kokeni. Licha ya kumtimua, walifungua kesi ili kudai
fidia kwamba alikuwa amekwenda kinyume na mkataba kwa kushindwa kuwatumikia
kutokana na kutumia mihadarati.
Gael Kakuta
Jina hili hutajwa karibu kila wakati orodha ya magarasa yaliyotokana na
wachezaji kutoka akademia ya Chelsea inapotolewa. Akiwa na umri mdogo alitoka
Lens ya Ufaransa hadi London 2007 na aliwasababishia Chelsea matatizo, kwani
walifungiwa kusajili, kisha marufuku hiyo ikaondolewa lakini akaishia kucheza
mechi sita tu za ligi.
Huyu aliathiriwa pia na mfumo wa Chelsea wa kuingiza na kuondoa makocha
na alizungushwa kote Ulaya kwa mkopo kabla ya kiangazi hiki kutupwa Sevilla.
Hata hivyo, si haki kwake kuwekwa kwenye kundi moja kama akina Torres na
Shevchenko kwa sababu bado ana umri wa miaka 24 tu; labda atafufua soka yake
siku zijazo.
Robert Fleck
Kabla ya Torres na Shevchenko, au hata Sutton, alikuwapo mtu anayeitwa
Robert Fleck. Chelsea walifungua zama mpya za Ligi Kuu ya England kwa kuvunja
rekodi kwa kutoa pauni milioni 2.1 kumsajili mshambuliaji huyo wa Norwich mwaka
1992.
Ikatokea kuwa kituko, kwani Fleck alifunga mabao manne tu katika mechi
48 akiwa na Blues.
Khalid Boulahrouz
Huyu alisajiliwa kutoka Hamburg, Ujerumani 2006 kwa pauni milioni nane
mwaka 2006. Mdachi huyu alipachikwa jina la ‘mla watu’ na kabla ya kuingia hapo
alikuwa bechi mahiri.
Alipendwa na kuheshimiwa; akapewa jezi maarufu namba tisa lakini baada
ya mechi 13 tu ligi kuu na kuonekana hana lolote alipelekwa Sevilla kwa mkopo
kabla ya kutupiwa virago moja kwa moja 2008.
No comments:
Post a Comment