Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 9, 2015

KUMEKUCHA LIGI KUU ENGLAND:



Nguvu ya Arsenal na jibu la Sterling kwa City

*Chelsea watazuilika? Man United kitaeleweka?


MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) unaanza huku timu zikiwa na mabadiliko kadhaa.
Arsenal wanakuja wakiwa kwenye kiwango kizuri kilichodhihirishwa na mechi za ziara ya kabla ya msimu, wakijilundikia makombe matatu.

Manchester City bado kwenye beki
Tuanze na Manchester City walioshinikiza hadi kufanikiwa kumsajili mshambuliaji kinda wa kati wa Liverpool, Raheem Sterling (20).
Sterling anadhaniwa atawasaidia City kutatua matatizo kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa kasi, ujana, na mchezaji wa England.
Ndiyo maana City walilipa pauni milioni 49 kama ada kwa Liver lakini pia na Sterling mwenyewe akalamba mkataba ambao atalipwa pauni milioni 47. Ni wazi atawaimarisha City haraka.
Hata hivyo, kuna maswali mengine yanabaki bila majibu – nani ni mshirika wa nahodha Vincent Kompany kwenye ulinzi?
Uhuishaji wa kikosi hiki uko wapi wakati mabeki wote wanne pale nyuma wameshafikisha umri wa miaka 30? Sterling ni mzuri lakini yeye mwenyewe atamudu kuwapandisha City?

Arsenal watatoa ushindani wa kweli EPL?
Arsenal ambao walifanikiwa kuwafunga Chelsea 1-0, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Arsene Wenger katika mechi 14 zilizopita dhidi ya Jose Mourinho, wamejilundikia makombe matatu ya ‘kishikaji’.
Je, watafanikiwa safari hii kuwa washindani wa kweli wa ubingwa wa England? Watamudu hilo wakiwa na Olivier Giroud kama tegemeo lao kwenye upachikaji mabao?
Walimtaka Karim Benzema lakini kocha wa Real Madrid, Rafa Benitez amewaambia wasahau hilo. Je, hakuna mwingine ambaye angefaa kuongezwa hapo kama alivyoshauri mkongwe wa Arsenal, Thierry Henry?
Anasema ili kutwaa ubingwa, Arsenal wanahitaji mpachika mabao wa kiwango cha juu kabisa. Giroud amefanya kazi kubwa na utumishi mwema katika misimu mitatu iliyopita, lakini utafiti unaonesha kwamba si rahisi awafikie akina Diego Costa, Sergio Aguero wala Robin van Persie. Sasa timu nyingine zikiwa na wapachika mabao wakali ni vigumu kwa Giroud kuwazidi. Labda wategemee nguvu ya Alexis Sanchez, Theo Walcott kama atakuwa na utimamu wa mwili kwa muda mwingi na Alex Oxlade-Chamberlaini anayetaka kuwa na msimu mzuri ujao.

Manchester United watarejesha heshima?
Klabu hii ipo kwenye kipindi cha mpito, wakijaribu bado kusimama tangu waondokane na kocha Alex Ferguson.
Chaguo na mrithi wake, David Moyes alishuhudia akiwaporomosha hadi nafasi ya saba mwisho wa msimu, akaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Louis van Gaal ambaye anaifumua na kuifuma upya United.
Zama za wachezaji wa England kung’ara zinaelekea kuisha, kwani naye anaonekana kwenda kwao na kulundika wachezaji. Anajiamini, anachukua hatua akishafanya uamuzi na ndiyo maana aliwatupia virago Van Persie na Radamel Falcao.
Analaumiwa kumuuza kwa Arsenal Danny Welbeck lakini yeye anasonga mbele akisema hata David De Gea kama vipi bora aondoke kwa sababu ya msigano unaoendelea, mwenyewe akitaka kurudi kwao Madrid, akachezee Real Madrid wanaomhitaji.
United walionekana kuwa watupu kwenye kiungo kwa miaka michache iliyopita na hiyo ndiyo tofauti yao na timu nzuri zaidi England na Ulaya. Viungo wao walikuwa wazito na vijeba mno kiasi cha kupitwa na wale wa Manchester City na Chelsea. 
Huenda sasa yakawapo mabadiliko, hasa baada ya usajili wa Morgan Schneiderlin kutoka Southampton na Bastian Schweinsteiger wa Bayern Munich, wote wakiwa na nguvu, uzoefu na wenye kujiamini.
Wakiungana na Michael Carrick na Ander Herrera, wanatakiwa kuipaisha timu, kudhibiti mchezo na kuwa na kiwango kizuri kwa ujumla. Kazi ipo kwa LVG kujua jinsi ya kuwapanga.
Hata hivyo, kocha wa Barcelona, Joseph Guardiola anasema kwamba Schweinsteiger hajapata kuwa na utimamu unaotakiwa wa mwili katika miaka mitatu iliyopita, pengine ndiyo sababu alikubali kumuuza.

Chelsea watakamatika msimu huu?
Baada ya shika nikushike ya msimu wa 2013/14, msimu ulipita ulikuwa na ushindani dhaifu zaidi kiasi cha Chelsea kwenda kwa mserereko kutwaa ubingwa, licha ya kutangatanga kwao katika mechi za mwisho.
Waliwazidi wenzao hapo juu pamoja na Liverpool na Southampton kwa mbali hivyo kwamba walifika mahali wakawa kama mwanariadha aliyefika karibu na mstari wa mwisho kisha akaamua kuketi kusubiri wenzake.
Arsenal na klabu za Manchester wasipojirekebisha na kulianzisha mapema, Chelsea wanaweza kufurahia tena, japokuwa dhamira kubwa inaonekana hata kutoka kwa Liverpool, hasa kwa kusajili ‘lundo’ la wachezaji.
Mwisho wa msimu uliopita, kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alisema kwamba msimu huu utakuwa mgumu kutokana na tamaa ya timu nyingine kutaka kuwapokonya kombe.
Anamtegemea sana nahodha na beki wake wa kati, John Terry ambaye hata hivyo si jambo la ajabu iwapo msimu utamkataa kwa sababu umri wake unakwenda.
Gary Cahill yupo na jitihada za kumpata John Stones wa Everton hazina uhakika wa kufaulu, na hata akiwapo Stones, uwapo wa tu tofauti na Terry ambaye Benitez alipata kumweka benchi akidai ni mzee mambo ni tofauti.
Wanamtegemea sana Diego Costa katika ushambuliaji na hata walimchezesha pale anapokuwa na tatizo kidogo la utimamu wa mwili.
Alikosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal kwa sababu misuli yake ya paja imeanza tena matatizo kama ilivyokuwa msimu uliopita. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi na hapo Chelsea watasikitika.
Pengine Mourinho atamtegemea zaidi mchezaji wake mpya aliye hapo kwa mkopo kutoka Monaco, 
Radamel Falcao aliyeahidi kumnoa na kumrejesha kwenye makali yake ya zamani, baada ya kuvurunda akiwa na Manchester United msimu uliopita.

Karata za Rodgerz zasubiriwa Liverpool
Msimu wa 2013/14 ulielekea kuwapa ubingwa Liverpool kama si kuvurunda katika mechi zao tatu za mwisho na kushindwa na Man City.
Ulikuwa msimu wa mwisho kabla ya kumuuza Luis Suarez kwa Barcelona, pengo ambalo hata sasa hawajaweza kuliziba licha ya kusajili wachezaji wengi, wakiwamo washambuliaji.
Kiangazi hiki wamempoteza Sterling wakati Daniel Sturridge anaendelea kujiuguza na huwa anaumia mara kwa mara. Msimu uliopita walifunga mabao karibu 60 pungufu yale ya msimu aliomalizia Suarez. Wamemaliza ligi wakiwa nafasi ya sita na wakichapwa mabao sita na Stoke.
Wamefanya usajili na matarajio ni kwamba Christian Benteke aliyesajiliwa kwa pauni milioni 32 kutoka Aston Villa atakuwa mtu wao muhimu pale mbele. Kuna Roberto Firmino aliyesajiliwa kwa ajili ya kiungo cha ushambuliaji kwa pauni milioni 29 kutoka Hoffenheim. 
Yupo Danny Ings aliyeonesha makali msimu uliopita kabla kocha Brendan Rodgers hajamsajili.

Timu zilizopanda daraja zina mtihani
Timu tatu zilishuka daraja msimu uliopita, moja ikiwa ndio kwanza ilikuwa imepanda, Burnley. Walibaki na kikosi kilichopanda lakini hakikumudu makeke, kimeshuka.
Queen’s Park Rangers (QPR) ni wengine walioshuka baada ya kupanda msimu mmoja kabla, wakiwa pia walikuwa wameshuka msimu mmoja tu kabla chini ya kocha Harry Redknapp.
Mwaka huu Norwich wamerudi EPL wakiwa na kikosi kile kile walichokuwa nacho huko chini na si tofauti sana na kilichoshuka daraja.
Wapya wengine ni Watford ambao wamesajili majina mapya katika kujiimarisha. Bournemouth ndiyo mara yao ya kwanza wanaingia EPL na wamekuja na maingizo machache mapya nay a maana. Tusubiri tuone kama watamudu kupata walau nafasi za kati za msimamo wa ligi.

No comments:

Post a Comment