Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 9, 2015

ARSENAL BADO INAHITAJI KUSAJILI WACHEZAJI WAWILI


ARSENAL inahitaji kusajili wachezaji wawili zaidi kuwa katika nafasi nzuri ya kushindania ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu.

Kwa msingi huo naenda tofauti kidogo na maoni ya nguli wa zamani wa klabu hiyo anayesema mara kwa mara kuwa wanahitaji kusajili kila idara ili kuweza kushindana na Chelsea, Manchester City na Manchester United kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa.

Tayari Profesa Arsene Wenger ameimarisha eneo moja la golikipa kwa kumsajili Petr Cech kutoka Chelsea na kipa huyo alionesha uwezo mkubwa kwenye mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya timu yake ya zamani ambapo Arsenal ilishinda kwa bao 1-0.

Cech alionesha utulivu langoni, alikuwa kama kiongozi na zaidi aliwanyima Chelsea mabao ya wazi kutokana na umahiri wake kiasi cha kuthibitisha kuwa kweli Arsenal ilihitaji mtu wa aina yake katika eneo hilo.

Kwa mtazamo wangu Arsenal bado inahitaji kusajili mfumania nyavu mahiri na zaidi kiungo mkabaji atakayesaidiana na Francis Coquelin ambaye kama Petr Cech naye alikuwa imara katika eneo la kiungo kiasi cha kuwapoteza Nemanja Matic,  Ramires na Francesc Fabregas.

Ushindi wa mabao 2-0 kwenye Ligi Kuu dhidi ya Manchester City, ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Manchester United  kwenye Kombe la Chama cha Soka cha England (FA) na sasa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chelsea kwenye Ngao ya Hisani ni uthibitisho tosha kuwa Arsenal wako tayari kabisa kwa mbio za ubingwa msimu ujao.

Moja ya shida kubwa ya Arsenal miaka kadhaa iliyopita ilikuwa ni kupata ushindi kwenye mechi kubwa kama dhidi ya Manchester United, Manchester City na Chelsea, shida hiyo sasa inaonekana kuondoka na kuelekea zama mpya.

Wenger anafahamika kuwa bado yuko sokoni akiwinda saini ya mfumania nyavu mahiri atakayepatikana hasa Karim Benzema kutoka Real Madrid, lakini binafsi namuongeza na Wiliam Calvarhlo kutoka Sporting Lisbon ya Ureno.

Arsenal inahitaji watu hawa wawili ili wasiendelee tena kusubiri zaidi mafanikio hasa ya kunyakua taji la Ligi Kuu ya  England ambalo ndio hasa kiini cha Arsene Wenger kushambuliwa mara kwa mara na Jose Mourinho.

Haihitaji zaidi ya maeneo hayo kwani tayari ina timu iliyokaa pamoja kwa muda mrefu na muunganiko wa kitimu ndio kitu cha msingi zaidi kuliko kununua lundo la wachezaji na kuwauza baada ya msimu mmoja.

Hakuna msimu ambao Aaron Ramsey ama Jack Wilshere hawawi majeruhi na ndio msingi wa Wenger kutakiwa kuleta kiungo mkabaji atakayeweza kucheza kama nyota hao wawili watakapokuwa majeruhi. Lakini kwa eneo la ushambuliaji bado inahitaji mtu atakayeweza kufunga mabao 20 kwa msimu.

Akipatikana mshambuliaji wa aina hiyo ataweza kusaidiana na akina Alexis Sanchez na Olivier Giroud na kuhitimisha ukame wa kushinda taji la Ligi Kuu ya England ambalo mara ya mwisho ni msimu wa mwaka 2002/2003. Kinyume chake bado ataendelea kusubiri na kutoa mwanya kwa hasimu wake mkubwa Jose Mourinho kumshambulia.

No comments:

Post a Comment