Timu ya Taifa ya wanawake ‘Twiga
Stars’ ipo kambini kwenye hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ikifanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuelekea nchini
Congo Brazzaville kushiriki michuano ya All Africa Games ambapo timu
hiyo ilifuzu kwa kuiondosha Zambia ‘Shepolopolo’ na kukata tiketi ya
kushiriki michuano hiyo.
Kocha mkuu wa timu hiyo Rogasian
Kaijage alikuwa ameomba aandaliwe mazingira kwa ajili ya kuiandaa timu
hiyo kwa muda mrefu kwa kuwaweka wachezaji kambini kwa vipindi tofauti
huku wakipata michezo kadhaa ya kirafiki ya kimataifa lakini mambo
yamekuwa magumu kutokana na hali ya uchumi kutoruhusu hayo yote
kufanyika.
Timu hiyo iliingia kambini Julai
15 mwaka huu ikiwa na mchanganyiko na timu ya vijana ambao walikuwa
wanajiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Zambia na baada ya wachezaji
wa timu ya vijana kwenda Zambia, wachezaji waliobaki waliendelea na
mazoezi chini ya mwalimu aliyebaki. Baadae, wachezaji wa timu hiyo
waliruhusiwa kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura na baadae
kurudi tena kambini baada ya siku tatu.
Awali mwalimu aliomba timu hiyo
ipelekwe Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi huko lakini pia hilo
limeshindikana kutokana na ukosefu wa fedha ambapo timu hiyo ilitegemewa
kuondoka kuelekea visiwani Zanzibar humo.
Lakini Kaijage amesema yeye
anaendelea na ratiba yake ya mazoezi kama alivyoipanga licha ya
kushindwa kwenda Zanzibar kuweka kambi huko japo amesema jambo hilo
linaweza linaweza kuwaathiri kisaikolojia baadhi ya wachezaji kwasababu
walikuwa wanajua wataenda kukaa mahali fulani na walikuwa
wamefurahia jambo hilo.
Amesema kambi ya Karume sio nzuri
sana kutokana na eneo kuwa na mwingiliano mkubwa na watu wengine
pamoja na mashabiki ambao huenda kuangalia mazoezi ya timu nyingine
zinazoutumia uwanja huo kwa ajili ya mazoezi.
Twiga Stars haina mdhamini kama
ilivyo Taifa Stars, Twiga inategemea kila kitu kutoka TFF. Ikumbukwe
timu hii inaenda kushiriki michuano mikubwa ya Afrika na itakutana na
timu zenye majina makubwa barani Afrika ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya
kupambana kutwaa ubingwa.
Kwa namna inavyoandaliwa timu hii
haioneshi kama tunataka kwenda kuleta changamoto kwenye mashindano hayo
mbali na kushiriki kisha kurejea nyumbani. Kuna haja kubwa ya kuwekeza
kwenye soka la wanawake kwasababu wameonesha wanaweza na ndio maana
wamefuzu kushiriki kwenye fainali hizo.
Timu itakapofanya vibaya lawama
zote zitaelekezwa kwa kocha na yeye ndie atakaeubeba mzigo wa lawama
zote endapo timu hiyo itafanya vibaya, lakini kuna swali la kujiuliza
kabla ya kumlaumu kocha wa Twiga kama timu haitafanya vizuri, tumewekeza
kwa kiasi gani kwa Twiga Stars mpaka tunataka matokeo mazuri?
Baada ya kupata jibu la swali hilo hapo ndipo tuanze kumnyooshea kidole kocha kwa matokeo mabovu atakayoyapata akiwa huko.
Wachezaji wengi wa Twiga hawana
timu na Tanzania hakuna ligi ya wanawake hivyo wachezaji hao walitakiwa
kukaa kambini kwa muda mrefu na kupata mechi nyingi za kirafiki za
kimataifa na timu zenye uwezo sawa au unaokaribiana na timu ambazo Twiga
itaenda kupambana nazo kwenye michuano ya All Africa Games.
Tanzania ipo kundi A pamoja na
Conco Brazzaville ambao ndio wenyeji wa michuano hiyo, Nigeria na Ivory
Coast. Congo, Tanzania na Ivory Coast ni timu ambazo zinashiriki
michuano hiyo kwa mara ya kwanza wakati Nigeria inashiriki michuano hiyo
kwa mara ya tatu na imewahi kutwaa medali ya dhahabu mara mbili mwaka
2003 na 2007.
No comments:
Post a Comment