KOCHA wa timu ya Taifa ya wanawake, ‘Twiga Stars’ Rogasian Kaijage
na nahodha wa timu hiyo Sophia Mwasikili wameahidi ushindi kwenye mchezo wa
kutafuta kufuzu fainali za wanawake barani Afrika utakaochezwa jumapili nchini
Zambia.
Twiga ambao wameingia hatua ya pili kutokana na kuwa kwenye nafasi
za juu kwenye viwango vya ubora barani Afrika itakuwa na kibarua kigumu ugenini
dhidi ya Zambia ambao ndio waliowaondoa kwenye mashindano hayo mwaka jana.
Akizungumza na wandishi wa habari wakati wakiagwa na Katibu wa
Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Selestine Mwesigwa, Kaijage alisema ana
kikosi kizuri na chenye hari ukilinganisha na mwaka jana kwani wamepata muda wa
mafunzo wa kutosha.
“Mwaka huu nina kikosi kizuri na chenye ari tofauti na mwaka jana
na nimepata muda wa kutosha wa kuwafundisha japo sikupata mechi za kimataifa za
kirafiki lakini nimetumia njia mbadala kuhakikisha nafanikisha lengo langu”,
alisema Kaijage.
Naye nahodha wa timu hiyo, mkongwe Sophia Mwasikili alisihi
watanzania wakuwaombea dua ili wapate ushindi na wao watafanya kila wawezalo na
kutumia ujuzi ambao kocha amewapa kuhakikisha wanapata ushindi.
Twiga Stars itaondoka kesho alfajiri na ndege ya Shirika la Ethiopia
‘Ethiopia Airways’ na itapitia Ethiopia
ikiwa na msafara wa watu 25 ambao ni na Blassy Kiondo (Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji), Beatrice Mgaya (kiongozi msaidizi), Rogasin Kaijage (kocha mkuu),
Nasra Juma (kocha msaidizi), Furaha Francis (Meneja), Christine Luambano
(Daktari) na Mwanahamis Abdallah (Mtunza vifaa).
Wachezaji ni Asha Rashid, Mwajuma Abdallah, Mwanahamis Omar,
Donisi Minja, Amina Bilal, Fatuma Bashiri, Esther Chabruma, Shelda Mafuru,
Maimuna Kaimu, Najiat Abbas, Stumai Abdalla, Fauma Issa, Thereza Yona, Fatuma
Hassan, Fatuma Omary, Sophia Mwasikili, Fatuma Khatibu na Etoe Mlenzi.
No comments:
Post a Comment